Klabu ya Dodoma jiji FC imethibitisha kuachana na Kocha Mkuu kutoka nchini Marekani Melis Medo baada ya kufikia makubaliano ya kuvunja mkataba.
Maamuzi ya Uongozi wa Dodoma jiji FC ya kuachana na Kocha huyo yalitangazwa usiku wa kuamkia leo na kuanikwa katika taarifa maalum iliyosainiwa na Katibu Mkuu wa klabu hiyo inayoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara.
Sababu kubwa iliyotajwa katika taarifa hiyo ni kumpa muda wa kutosha kocha huyo mwenye asili ya nchini Misri kushughulikia changamoto za kifamilia zinazomkabili.
“Uongozi wa timu ya Dodoma Jiji FC inayomilikiwa na Halmashauri ya Jiji la Dodoma unapenda kuujulisha Umma kuwa umefikia makubaliano ya pande mbili kusitisha mkataba na aliyekuwa Kocha
Mkuu Ndugu Medo Melis ili Kocha apate muda wa kutosha kushughulikia changamoto za kifamilia zinazomkabili.
Uongozi wa Dodoma Jiji unatoa shukrani za dhati kwa Kocha Medo kwa mchango wake ndani ya Klabu yetu na tunamtakia kila lenye heri katika majukumu hayo ya kifamilia.
Aidha, tunapenda kuwajulisha kuwa mchakato wa kupata Kocha Mkuu mpya umeanza na unatarajiwa kukamilika hivi punde.” Imeeleza taarifa ya Dodoma jiji FC