Katika vigogo watatu ambao walihojiwa na kamati ndogo ya maadili na usalama wa chama cha mapinduzi (CCM), Katibu Mkuu msaafu wa chama hicho amekuwa kigogo wa pili kuomba msamaha na kumuacha kada Bernard Membe pekeyake ambaye amefutwa uanachama.
Jana, Kinana alimwangukia na kumuamba radhi Rais John Magufuli kwa yote aliyomkwaza na kumhuzunisha, jambo lililo pelekea kusimamishwa kujihusisha na siasa kwa miezi 18.
Akizungumza na Azam tv, Kinana alisema kuwa wakati fulani alihuzunika na kukasirika na kujikuta akienda mbali kidogo na kusema maneno ambayo labda hayakuwa mazuri kwa mwenyekiti wake, Rais Magufuli.
” Baada ya kutafakari, nadhani naweza kusema labda ni wakati mwafaka, ni wakati mzuri nami kuungana nao na kumtaka radhi mwenyekiti na kumwomba msamaha” amesema Kinana.
Ikumbukwe kuwa, Julai 14 , 2019, Kinana na Makamba waliandika barua kwenda kwa Katibu wa baraza la ushauri la viongozi wastaafu wa chama hicho, Pius Masekwa kulalamikia udhalilishwaji unaofanywa na kada mwenzao Cyprian Musiba.
Vigogo hao walikuwa wakilalamika kwamba Musiba amekuwa akitoa kauli kama Kinana na Makamba wanamhujumu Rais Magufuli ili awe Rais wa awamu moja jambo ambalo walidai sio kweli.
Mzozo mwingine ambao alihusika Kinana, ni ule uliosababishwa na udukuzi wa sauti zinazodaiwa kuwa ni za Kinana, Makamba, na Membe.
Wengine ambao walidukuliwa wakimsema vibaya Mwenyekiti wao Magufuli ni Nape Nnauye, William Ngeleja na January Makamba ambao kwa nayakati tofauti waliomba msamaha.
Katika makosa hayo ya kinidhamu, Membe pekee ndiyo bado hajaomba msamaha ambaye Februari 28 mwaka huu alivuliwa uanachama.