Aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Serikali ya Awamu ya Nne, Bernard Membe ameitwa na Kamati ya Udhibiti na Nidhamu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa ajili ya kuhojiwa katika kikao kitakachofanyika Februari 6, 2020.
Desemba mwaka jana, Kamati hiyo ya CCM ilitangaza kuwa watamhoji Membe na Makatibu Wakuu wa zamani wa chama hicho, Abdulrahman Kinana na Yusuf Makamba kutokana na mienendo yao.
Majina ya Makatibu wakuu hao yalitajwa baada ya kuvuja kwa sauti za mawasiliano yao ya simu wakionekana kubeza mwenendo wa chama hicho na mpasuko unaoweza kutokea. Wengine waliohusishwa na sakata hilo lakini baadaye waliomba radhi na kusamehewa na Mwenyekiti wa chama hicho, Rais John Magufuli ni January Makamba (Mbunge wa Bumbuli), Nape Nnauye (Mbunge wa Mtama) na William Ngereja (Mbunge wa Sengerema). Watatu hao wamewahi kuwa Mawaziri.
Kupitia mtandao wa Twitter, mtu anayetumia jina la Bernard Membe na husadikika kuwa ndiye Membe halisi ameandika, “Hatimaye jana jioni nimepokea barua ya kuitwa kwenye kikao cha kamati ndogo ya udhibiti na nidhamu jijini Dodoma.
“Kikao kitafanyika Februari 6, 2020 saa tatu asubuhi kwenye jengo la White House. Nitahudhuria bila kukosa na bila kuchelewa! Stay tuned,” Membe aliongeza.
Mwaka jana, Katibu Mkuu wa chama hicho, Dkt. Bashiru Ally alieleza kutopendezwa na mienendo ya Membe. Alisema tangu kumalizika kwa uchaguzi wa mwaka 2015 hajawahi kuonekana katika shughuli zozote za chama, hivyo alimtaka afike ofisini kwake.
Hata hivyo, Membe hakuukubali wito huo uliotolewa na Katibu Mkuu wake katika mkutano wa ndani, Mkoani Geita, alisisitiza kuwa kuna njia na utaratibu rasmi wa kuitana ndani ya chama hicho ambao alidai haukufuatwa.
Sasa ni rasmi, atahojiwa na Kamati hiyo na huenda kila kitu kikawa hadharani.