Meneja wa Vinara wa Ligi Kuu ya England Arsenal, Mikel Arteta amemtaka mshambuliaji wake kutoka nchini Brazil Gabriel Jesus kupigania nafasi ya kucheza kwenye kikosi cha kwanza katika michezo yote ilizosalia.
Arteta amefunguka hilo, kwa lengo la kumuweka wazi Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 25, kutokana na upatikanaji wa nafasi katika kikosi cha The Gunners, ambacho kwa sasa kina wachezaji wengi wenye sifa za kuanza.
Mshambuliaji huyo wa The Gunners alicheza mchezo wake wa kwanza tangu alipofanyiwa upasuaji wa goti mwezi Desemba mwaka jana, akitokea benchi katika kipindi cha pili kwenye ushindi mnono wa 3-0 dhidi ya Fulham mwishoni mwa juma lililopita, na wababe hao wa London kurudisha pengo la alama tano kileleni mwa Msimamo wa Ligi dhidi ya Man City.
Kurudi kwa Jesus utakuwa ni msaada mkubwa kwa Arteta katika kufanya uchaguzi wakati timu yake ikiendelea kupambana kuwania ubingwa wa kwanza tangu msimu wa 2003/04.
Arteta amesema: “Ilikuwa hatua yake ya kwanza. Hatukujua kama ulikuwa mchezo sahihi lakini nilimtazama machoni mwake na akasema niko tayari.”
“Sasa anahitaji kupambania nafasi yake, kama mchezaji mwingine yeyote.”
Gabriel Jesus alisajiliwa Arsenal mwanzoni mwa msimu huu akitokea kwa mabingwa watetezi wa England Machester City, huku akicheza michezo kumi na tano na kufunga mabao matano.