Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel amesema atabaki nje ya kinyang’anyiro cha muungano wake wa vyama vya siasa za wastani vya mrengo wa kulia kuhusu nani anayepaswa kuwa mgombea wa kuirithi nafasi yake.
Wagombea wawili wa majimbo, Armin Laschet kiongozi wa chama cha Merkel cha Christian Democratic Union – CDU na Markus Soeder kiongozi wa chama kidogo ndugu cha jimbo la Bavaria wanajiandaa kuwasilisha nia yao ya ukansela kwa wabunge.
Chama cha Christian Social Union – CSU nacho kimetangaza rasmi Jumapili nia yao ya kugombea baada ya miezi kadhaa ya kushambuliana hadharani.
Alipoulizwa kama ana wasiwasi kuwa uhasama wa viongozi hao unaweza kuhujumu umoja wa muungano wao na hata kuufanya upoteze umaarufu, Merkel ameweka wazi kuwa hatoingilia siasa hizo za mpambano.
Uchaguzi wa Bunge la Ujerumani unaotarajiwa kufanyika Septemba 26, mwaka huu utaamua nani atakayemrithi Merkel ambaye hatogombea kwa muhula wa tano baada ya karibu miaka 16 madarakani.