Nahodha na mshambuliaji wa FC Barcelona Lionel Messi, amefichua siri ya kushindwa kuonesha kiwango maridhawa msimu huu, na kuisaidia klabu hiyo kuwa tishio kama ilivyozoeleka, kulingana na matokeo ya misimu iliyopita.
Messi amesema jaribio lake la kutaka kuondoka klabuni hapo ambalo liligonga mwamba wakati wa usajili wa majira ya kiangazi mwaka huu, limemuathiri kwa kiasi kikubwa.
Mwezi Agosti mwaka huu mshambuliaji huyo kutoka nchini Argentina alidhamiria kutumia kifungu cha sheria katika mkataba wake ambacho kingemwezesha kuondoka katika klabu hiyo, lakini viongozi wa FC Barcelona walikataa, kwa kuweka wazi endapo angeondoka ada yake ya uhamisho ilipaswa kuwa Euro milioni 700 (sawa na Pauni milioni 624).
“Nilivuta kila kitu hadi mwanzo wa msimu,” amesema Messi mwenye umri wa miaka 33, alipohojiwa na kituo cha televisheni cha Hispania cha La Sexta.
“Ukweli ni kwamba sasa sina neno, lakini dirisha la uhamisho lililopita lilikuwa ni wakati mbaya sana.”
Hata hivyo Messi, anaweza kuondoka FC Barcelona bila malipo mkataba wake utakapokamilika mwisho wa msimu huu, na atakua uwezo wa kujadiliana na klabu nyingine kuanzia Januari mosi 2021.
Rais wa mpito wa Barcelona Carlos Tusquets, ambaye alichukua nafasi ya uongozi wa klabu hiyo hadi uchaguzi utakapofanywa mwezi Januari baada ya Josep Maria Bartomeu kujiuzulu Oktoba, amesema
“Kulingana na tathmini ya kifedha ” Messi angekuwa ameuzwa katika dirisha la uhamisho lililopita.”
Wachezaji wa FC Barcelona walikubali kupunguziwa marupurupu mwezi Novemba ili kuwawezesha washindi hao mara 26 wa taji la La Liga kuokoa Euro milioni 122 (£110m).
“Kwa sasa najihisi vyema na natarajia kukabiliana vilivyo kushinda katika kila shindano lililopo mbele yetu. Nafahamu klabu inakabiliwa na hali ngumu kwa sasa katika ngazi ya usimamizi, uwanjani na kila kitu kinachozunguka Barca kwa sasa ni kigumu, lakini najihisi mwenye furaha,” amesema Messi.
Messi alifikia rekodi ya mchezaji mkongwe wa Brazil, Pele, ya kufunga mabao 643 ndani ya klabu kwa kuisawazishia Barcelona bao lililoiwezesha kutoka sare dhidi ya Valencia siku ya Jumamosi.
Lilikuwa bao la tisa katika michezo 17 ya FC Barcelona, ambao wako nafasi ya tano katika msimao wa Ligi Kuu ya Hispania (La Liga).