Nahodha na mshambualiji wa FC Barcelona Lionel Messi huenda akaondoka klabuni hapo, kufuatia siri nzito iliyofichuliwa na kiongozi wa zamani wa Inter Milan ya Italia, Massimo Moratti.
Moratti ambaye amewahi kuwa Rais wa Inter Milan amesema anaamini klabu za Ligi Kuu Italia ‘Serie A’ zinajaribu kupigania saini ya mshambuliaji wa Kiargentina Lionel Messi kutoka Barcelona hata kama hakuna uwezekano wa kutua huko.
Amesema Inter Milan ‘Nerazzurri’ ni miongoni mwa klabu ambazo zipo kwenye vita ya kumnasa nyota huyo kufuatia kuonyesha kwake dhamira ya kutaka kuondoka Camp Nou.
Moratti ambaye aliiongoza klabu hiyo ya mjini Milan kati ya 1995 na 2013, anafikiri kwamba tangazo la hivi karibuni ambalo lilionekana katika runinga likifanywa na wamiliki wa klabu hiyo kwenye kanisa kuu la Milan la Duomo ni ishara kwamba wako tayari kumleta San Siro.
“Sio operesheni rahisi kiuchumi, hiyo ni wazi. Lakini kizuizi kikubwa ni nia ya Messi. Lazima uelewe ikiwa anataka kutoka Barca kabisa.
“Nadhani Inter Milan tayari wamejaribu [kutaka kumsajili]. Nimeona tangazo hili linanifanya nifikirie kwamba pengine tayari kuna mpango umesukwa wa kuhakikisha anasajiliwa.
“Kama sivyo, nadhani watafanya hivi karibuni,” Moratti aliiambia AS.
Messi amekua na wakati mgumu siku za karibuni, hasa baada ya FC Barcelona kushindwa kufikia lengo la kutwaa ubingwa wa Hispania msimu wa 2019/20, huku wakitolewa kwa aibu kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya.
Kwenye michuano hiyo FC Barcelona walitupwa nje kwa kufungwa mabao manane kwa mawili dhidi ya FC Bayern Munich ya Ujerumani, ambao ndio mabingwa wapya wa Ulaya.