Mshambuliaji wa Klabu ya Barcelona, Lionel Messi amekiri kuwa bado anauguza vidonda vya kipigo cha Liverpool kwenye Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya akikitaja kuwa kipindi kibaya zaidi kuwahi kutokea kwenye maisha yake ya soka.
Akizungumza leo kwenye mkutano wake na waandishi wa habari, Messi mwenye umri wa miaka 31 amesema kuwa kipigo cha 4-0 walichokipata Mei 7, 2019 kilikuwa kizito na kwamba hadi leo amekuwa akikitafakari. Majogoo wa London walifunika matokeo ya 3-0 waliyokuwa nayo Barcelona kama mtaji kutoka nyumbani.
“Tunapaswa kuomba radhi hasi kwa jinsi tulivyocheza katika kipindi cha pili dhidi ya Liverpool, sio kwa sababu ya matokeo, lakini ni kwa sababu ya jinsi ilivyoonekana na kwamba hatukuwa tunashindana. Ulikuwa wakati mbaya zaidi kuwahi kutokea kwenye maisha yangu ya soka,” alisema na kuongeza, “tulipigwa vibaya na tulipigwa sana.”
Aidha, mchezaji huyo ameeleza kuwa ili kupunguza maumivu ya kipigo kile wanapaswa kushinda Kombea la Copa Rey.
“Tunapaswa kushinda Copa Rey, hiyo ndiyo itakuwa njia bora zaidi ya kuumaliza msimu huu,” aliongeza.
Mabingwa hao wa La Liga wanaweza kufanikisha ndoto yao kama watavuka kiunzi cha Valencia Jumamosi hii.
Messi ameonya kuwa endapo watafungwa tena Jumamosi hii timu itajisikia vibaya zaidi kuliko yote waliyowahi kuyafanya.