Kipimo cha mchezaji anayejitambua kuwa hawezi kushuka kiwango akiwa nje ya timu, atasimamia programu za mazoezi ya kumuweka fiti, ndicho anachokiishi kipa aliyesimamishwa, Metacha Mnata kuhakikisha hatoki kwenye mstari.
Amesema kinachomlinda ni programu alizokuwa anazifanya chini ya kocha wa makipa wa timu yake Razak Siwa, hivyo anaziendeleza muda ambao yupo nje ya timu, akisubiri hatma yake.
“Nafanya sana mazoezi ya kulinda kipaji changu, siwezi kubweteka kwasababu ya kuwa nje ya timu, kwani soka ni kazi yangu lazima nitazingatia kile kinachofanya niwe bora,”
“Mchezaji anayejitambua ni yule anayelinda kiwango chake akiwa nje ya mamlaka ya kocha, kwani anajua nini anapaswa kufanya na nini hapaswi kukifanya, hilo linakuwa linamrahisishia hata kocha kuwa na wachezaji ambao si wa kuwasukuma kufanya kazi,” amesema Metacha.
Uongozi wa Young Africans ulimsimamisha Metacha Mnata kwa muda usiojulikana, baada ya kulumbana na mashabiki kwenye mchezo wa Ligi Kuu dhidi Ruvu Shooting mwezi uliopita.
Mbali na kulumbana na mashabiki, Metacha aliwaonesha ishara ya matusi, hali iliyoibua taharuki kubwa kwa wadau wa soka nchini.
Pia TFF nayo imemuadhibu kutokucheza michezo mitatu mlinda mlango huyo, sambamba na kumtoza faini ya shilingi laki tano.