Kocha Mkuu wa Kagera Sugar Mecky Mexime amewataka washambuliaji wake kupambana ili kuiwezesha timu hiyo kufanya vizuri katika michezo minane iliyosalia kabla ya kufikia ukomo wa Ligi Kuu msimu huu 2022/23.
Kegera Sugar juzi Jumatatu (Februari 06) iliambulia sare ya bila kufungana dhidi ya Polisi Tanzania iliyokuwa nyumbani Uwanja wa Ushirika Moshi, mkoani Kilimanjaro.
Kocha Mexime amesema haridhishwi na mwenendo mbovu wa matokeo yanayowakabili kwa sasa, hivyo ni jukumu la kila mchezaji kuhakikisha anatimiza majukumu yake hususan katika eneo la ushambuliaji.
“Tangu alipoumia Anuary Jabir tumekuwa tukipata wakati mgumu, ila hatuwezi kujutia hilo isipokuwa kazi iliyobaki ni kwa wengine kuonesha uwezo na thamani yao pindi mmoja wao anapokosekana.”
“Tumebakiwa na michezo minane na nafasi tuliyopo sio mbaya sana ingawa tuna uwezo wa kusogea juu zaidi, ni changamoto kubwa kwangu kama kocha ambaye anaendelea kuifanyia maboresho timu yangu siku baada ya siku.” amesema Mexime
Katika michezo minne iliyopita ya Ligi Kuu Tanzania Bara, Kikosi cha Kagera Sugar hakujafunga bao hata moja, hali ambayo inathibitisha ubutu wa safu ya Ushambuliaji ya klabu hiyo.
Kwa upande wa beki wa kikosi cha Kagera Sugar Detius Peter amesema watahakikisha katika michezo iliyosalia wanapata matokeo mazuri, licha ya kukiri ugumu uliopo kutokana na kila timu kupambana zaidi katika kipindi hiki cha kuelekea ukingoni mwa Ligi Kuu msimu huu.