Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita jana alikamatwa na jeshi la polisi kwa tuhuma za kufanya maandamano bila kuwa na kibali.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa jeshi hilo lilimkamata Meya huyo ambaye pia ni diwani wa Vijibweni akiwa anaandamana na wafuasi wake akidai kuwa anaenda kuzindua kisima cha maji.
Aidha, Kamanda Mambosasa amedai kuwa Meya huyo alitaka kupora sifa za ujenzi wa kisima hicho wakati kimejengwa na Serikali kupitia kwa Mkuu wa Wilaya.
“Yeye alikuwa anataka kupora ili kutafuta sifa kuwa alikijenga yeye wakati mradi ni wa Serikali, aliokuwa amewaalika walikimbia wote,” Kamanda Mambosasa anakaririwa na Mwananchi.
Wakati jeshi hilo likieleza kuwa litaendelea kumshikilia hadi upelelezi utakapokamilika, Chadema kupitia Ofisi ya Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje, imeeleza kuwa Meya huyo ambaye ni mwanachama wao alikuwa na mkutano na wananchi katika kata hiyo na kwamba baadaye alienda kuzindua matawi mapya.