Wakati Kikosi cha Mabingwa wa Soka Tanzania Bara kikitarajiwa kuondoka nchini kesho Alhamis (April 20) kuelekea nchini Nigeria kwa ajili ya mchezo wa Mkondo wa Kwanza wa Robo Fainali Kombe la Shirikisho Barani Afrika dhidi ya wenyeji wao, Rivers United, utakaochezwa Jumapili (April 23), mshambuliaji wa timu hiyo, Fiston Mayele, amesema wameshasahau matokeo yaliyopita dhidi ya Simba SC na akili yao ni michuano hiyo ya kimataifa.

Jumapili (April 16) Young Africans ilikubali kipigo cha mabao 2-0 kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya watani wao wa jadi Simba SC, huo ukiwa ni mchezo wa mwisho kwao kabla ya kuelekea Nigeria kwenye michuano hiyo ya kimataifa kwa ngazi ya klabu.

Mayele amesema hana shaka na mchezo huo kwani alikuwa anausubiria kwa muda mrefu na matokeo yaliyopita dhidi Simba SC ameyasahau na sasa anaelekeza nguvu zake katika mchezo huo.

Kwa upande wa Meneja wa Klabu ya Young Africans, Walter Harson, amesema baada ya mchezo wao wa Jumapili waliwapa mapumziko mafupi wachezaji wao na kwamba wataondoka nchini kesho Alhamisi (April 20) kuelekea Nigeria.

“Timu yetu inatarajia kuondoka Alhamisi kuelekea nchini Nigeria kwa ajili ya mchezo wetu huo, tunaamini tutafanya vizuri kutokana na maandalizi tuliyoyafanya,” amesema Harson.

Meneja huyo amesema hana wasiwasi na wapinzani wao hao kwani wamewafuatilia kipindi kirefu katika michezo yao waliyoicheza Aidha, alisema wachezaji wana morali ya juu kuelekea kwenye mchezo huo ambao unatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa.

Kwa upande wa Afisa Habari wa klabu hiyo, Ali Kamwe, ameelezea safari hiyo pamoja na kipigo ambacho timu hiyo ilikipata Jumapili iliyopita dhidi ya watani zao wa jadi Simba SC, akisema wachezaji wamejisikia vibaya.

Hata hivyo amesema tayari pambano limesha na akili yao sasa ipo kwenye mechi ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, pamoja na Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’.

Kamwe pia amewapongeza wanachama na mashabiki wa Young Africans kwa utulivu hata baada ya kupoteza mchezo huo, akisema ni watu waliokomaa kimichezo.

Wabunge wa Mbeya waibeba Mbeya City Ligi Kuu
Mapigano Sudan: Tanzania yaungana na Baraza la amani Afrika