Achraf Hakimi amekugeuka kuwa shujaa wa Africa kwenye Dunia ya soka baada ya kushinda penati iliyofanikisha timu ya taifa ya Morocco kuingia robo fainali za kombe la dunia 2022.
Morocco, inakuwa timu ya nne kutoka bara la Afrika kufikia robo fainali za kombe la dunia, ikitanguliwa na Cameroon (1990),Senegal (2002) na Ghana (2010).
Hakimi (24) ambaye ni nyota wa PSG alizaliwa na kukulia jijini Madrid, Hispania, wazazi wake ni wahamiaji kutokea Morocco,na nyota huyo ana uraia pacha.
Kuchezea taifa la Morocco ulikuwa ni uamuzi wake binafsi, hii ina maana kuwa hapo jana Jumanne (Desemba 06) alikuwa akicheza dhidi ya taifa lake la kuzaliwa.
Ni mtoto wa kwanza kwenye familia yenye watoto watatu. Baba yake alikuwa mfanyabiashara wa mitaani kama mmachinga na mama yake alikuwa akisafisha nyumba za watu. Alisajiliwa na Real Madrid Academy akiwa na umri wa miaka 8.
Familia yake ilikuwa na hali ngumu ya kifedha alipokuwa mdogo, ili kutimiza ndoto za kijana wao wazazi wake walifanya kazi mchana na usiku.
Juhudi zake kwenye soka ziliwafurahisha sana nao walipambana kumpatia mahitaji kama jezi na viatu vya kumfaa ili aendeleze ndoto hiyo.
Soka lilipomkolea alianza kupoteza hamu ya shule, mwanzoni wazazi wake hawakupenda suala hilo lakini baadaye walikubaliana naye.
Hakimi ana mke na watoto wawili wa kiume. Mkewe, Hiba Abouk (36) ni muigizaji maaruufu kutokea Hispania ambaye asili yake ni Libya na Tunisia.