Mwanamke mmoja aliyetambulika kwa jina la Mkami Shirima(33) mkazi wa Ilikiurei, nje kidogo ya jiji la Arusha, anadaiwa kumuua mfanyakazi wake wa ndani, Salome Zacharia (17) kwa kumpiga fimbo akimtuhumu kuiba Sh elfu 50.
Mwanamke huyo ambaye anashikiliwa na jeshi la polisi mkoani hapo, anadaiwa kutenda tukio hilo siku ya Alhamisi wiki iliyopita na baadaye alimfungia katika chumba kimoja wapo katika nyumba yake kwa muda wa siku mbili bila kumpatia chakula wala maji ya kunywa huku akiendelea kumchapa.
Akielezea tukio hilo mtoto wa mtuhumiwa huyo aitwaye, Sonia Bakari (17) amasema siku ya Alhamisi mama yake alikuwa anatafuta kisanduku cha kuhifadhia fedha (Kibubu) kilichokuwa na kiasi cha shilingi milioni 1.
Amesema kuwa mara baada ya kukikosa kisanduku hicho katika chumba chake alimuuliza marehemu pamoja na mtoto wake (Sonia) iwapo kama wamekichukua hata hivyo wawili hao walikana kukiona ndipo mama huyo alipoanza kumpiga marehemu.
Hata hivyo Sonia alimwambia mama yake kwamba aache kumchapa marehemu kwa kuwa yeye ndiye aliyekichukua kisanduku hicho na kukivunja na kutoa shingi laki moja na kumpatia sh. elfu 50 marehemu ili amtumie mama yake aliyeko kijijini Singida.
Sonia anadai kwamba licha ya kumweleza mama yake asiendelee kumwadhibu marehemu bado aliendelea kumchapa mfululizo huku damu zikimchuruzika na kisha kumfungia katika chumba kimoja wapo bila kumpatia huduma yoyote ya chakula.
“Nilimwambia mama asimpige Salome kwa kuwa mimi ndiye niliyekichukua hicho kisanduku na kukificha chumbani kwetu nilikivunja na kuchukua sh. laki moja na kubakiza sh. laki tisa na nilimpatia elfu 50 Salome ili amtumie mama yake na mimi nikabaki na Elfu 50” Amesema Sonia.
Amesema kuwa siku ya Jumamosi wifi yake (jina limehifadhiwa) alimweleza mama huyo kwamba marehemu alikuwa akitapika damu ndipo mama huyo aliamua kumpeleka katika hospitali ya mkoa ya Mount Meru na marehemu alifikwa na mauti siku iliyofuata Jumapili.
Kamanda wa polisi mkoani Arusha Jonathani Shanna amethibitisha tukio hilo na kueleza kwamba mwili wa marehemu umehifadhiwa katika hospitali ya mkoa Mount Meru ukisubiri uchunguzi wa daktari.
Mtuhumiwa atafikishwa mahakamani kujibu shtaka la mauaji linalomkabili.