Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Dkt. Omar Dadi Shajak amezitaka Halmashauri zilizonufaika na Mradi wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi kwa Kutumia Mifumo Ikolojia Vijijini (EBARR) kuusimamia vyema, ili uwe endelevu.
Shajak ametoa wito huo alipofanya ziara ya kukagua mradi wa EBARR unaotekeleza na Ofisi ya Makamu wa Rais kwa ushirikiano na Mfuko wa Mazingira wa Dunia (GEF) katika Halmashauri ya Mvomero mkoani Morogoro.
Katika ziara hiyo amekagua lambo na kilimo cha mbogamboga kwa umwagiliaji wa matone na shamba darasa la uyoga, ujenzi wa kiwanda kidogo cha bidhaa za ngozi, kisima kirefu na vitalu nyumba katika Kijiji cha Mingo.
Amesema, “kule kwetu ni kisiwa, uvuvi na utalii ni shughuli kuu na kupitia mradi huu vikundi vya uvuvi vilioatiwa boti kupitia EBARR na wao wakajiongeza siku ambayo hawavui wanasafirisha watalii kwenda kwenye visiwa kutalii na kupata fedha ambazo zimewasadiai kununua boti nyingine.”
Aidha, Dkt. Shajak amesema nia ya Serikali ya kuwapelekea wananchi miradi ni kuwasaidia waweze kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi kwa kufanya shughuli za kujiongezea kipato na wakati huo wanatunza mazingira.