Mwanamke mmoja ameokolewa akiwa amedhoofika msituni kutokana na makali ya njaa na kukimbizwa katika kituo cha Afya kwa matibabu mjini Malindi, huku maafisa wa Upelelezi wa jinai wakitambua makaburi 12 ya watu wanaodaiwa kuzikwa kwenye shamba la mhubiri tata Paul Makenzi.
Kwa mujibu wa taarifa ya Polisi mjini humo, imesema wanahofia kuwa kuna miili zaidi kwenye shamba hilo la ekari 800 na kutokana na amri ya kiongozi huyo wa Kanisa la Good news International kuwataka waumini wake kuingia katika mfungo wa kutokula na kunywa hadi wafe ili wakakutane na MUNGU.
Paul Mackenzie, Mhubiri wa Kanisa la Good News International
Mapema Wiki iliyopita, Mchungaji huyo aliondolewa dhamana aliyopewa, ambapo Hakimu Mkuu, Elizabeth Usui alisema mtuhumiwa huyo amekuwa akiendeleza vitendo vyake eneo la Shakahola – Kilifi, licha ya kuzuiliwa kufanya hivyo na kesi yake itatajwa tena Mei 2, baada ya uchunguzi kukamilika.
Watu wengine 11, walifariki April 13, 2023 kutokana na tukio hilo na Mtuhumiwa huyo Makenzie ambaye amekua akidaiwa kuendesha mahubiri yenye itikadi kali katike eneo la Shakahola, alifikishwa mahakama siku ya Jumatatu Aprili 17, 2023.