Baadhi ya wafanyakazi wa ofisi za Serikali nchini  Nigeria Jumanne wameanza mgomo kupinga  kupanda kwa gharama ya maisha baada ya kuondolewa kwa ruzuku ya mafuta, wakitishia kusimamisha shughuli zote kiutendaji.

Maelfu ya Wafanyakazi hao kupitia Chama cha Wafanyakazi cha Nigeria Labor Congress, walianza mgomo huo wa siku mbili, wakisema ni onyo kwa Serikali ukiwa wa pili chini ya miezi miwili wakimlalamikia Rais wao Bola Tinubu.

Vyombo vya Habari vya Nigeria, vimesema wawakilishi kadhaa kutoka vyama tofauti vya wafanyakazi waliomba wanachama wao wasiende kazini, huku baadhi wakifunga ofisi za Serikali ili kushiriki mgomo huo.

Hata hivyo, juhudi za kuzuia mgomo huo zilishindikana baada ya Viongozi wa vyama vya Wafanyakazi kukataa kuhudhuria mkutano ulioitishwa na Wizara ya Kazi huku Rais wa chama cha wafanyakazi, Joe Ajaero akisema watachukua uamuzi mwingine, iwapo Serikali haitatimiza matakwa yao ikiwemo nyongeza ya mishahara.

Aliyemwingilia Mgonjwa wa akili jela miaka 15
Tanzania mwenyeji jukwaa la Majaji Wakuu