Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja amesema maeneo ya Mapori Tengefu yatakayopandishwa hadhi kuwa Mapori ya Akiba ni maeneo yenye hadhi nzuri kwa ajili ya uhifadhi na hayana vijiji vya wananchi.
Ameyasema hayo leo Juni 20, 2022, Bungeni jijini Dodoma alipokuwa akijibu hoja ya Mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka alieuliza kama Serikali itayapandisha hadhi maeneo ya wananchi.
“Hotuba ya Waziri wa Maliasili na Utalii iligusia upandishwaji wa maeneo ambayo hayatahusisha vijiji vya wananchi, hivyo maeneo yanayokwenda kupandishwa hadhi kutoka mapori tengefu kuwa mapori ya akiba ni maeneo muhimu tu kwa ajili ya uhifadhi na hayana wananchi ndani yake.” amesisitiza Masanja.
Ameongeza kuwa maeneo hayo ya mapori tengefu kutokana na umuhimu wake kwa asilimia kubwa yanatumika kwa ajili ya shughuli za uhifadhi na utalii.
Amesema Serikali inapoona pori tengefu lina hadhi nzuri na sifa ya kuhifadhiwa zaidi kwa maslahi ya taifa hulipandisha hadhi kutoka pori tengefu kuwa pori la akiba vivyo hivyo pori la akiba linapoongezeka sifa linapanda kuwa hifadhi ya Taifa.
Masanja amewaomba wabunge wanaopakana maeneo hayo wawe na uelewa wa pamoja huku akisisitiza kuwa ardhi ni mali ya umma na si ya mtu mmoja akiwaomba waache kutumia kauli zinazoweza kuwagawa wananchi.