Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Mhandisi Kundo Mathew ametoa maelekezo kwa makampuni ya simu na wamiliki wa minara ya mawasiliano kuingia mikataba ya ulinzi wa minara ya mawasiliano na Serikali ya kijiji katika eneo husika.
Mhandisi Kundo ameyasema hayo wakati wa ziara yake ya kikazi katika Wilaya ya Newala mkoani Mtwara ya kukagua ujenzi, uwezo na ubora wa minara ya mawasiliano ambapo alikutana na malalamiko ya malipo ya mlinzi katika mnara wa tigo uliopo katika Kijiji cha Mdimba pamoja na changamoto ya mawasiliano ya mtandao wa tigo kutokana na mnara huo kutumia nishati ya mwanga wa jua pekee.
Sambamba na hilo, Mhandisi Kundo amewaagiza Wakuu wa Wilaya nchini ambao ndio wenyeviti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama katika maeneo yao kuhakikisha mtoa huduma yeyote mwenye mnara wa mawasiliano ndani ya wilaya zao anaandikiwa barua ya kufanya makubaliano mapya na kusainishana mikataba ya ulinzi wa minara na Serikali ya kijiji ambacho mnara upo.
“Kuanzia sasa watoa huduma wote watakuwa wanaingia mikataba ya ulinzi wa minara na Serikali ya Kijiji husika ambayo ndio itawajibika kuhakikisha eneo la mnara linakuwa na ulinzi muda wote, utaratibu huu umekuwa ukitumiwa na Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) bila kuleta changamoto wala malalamiko ya aina yeyote”, alizungumza Mhandisi Kundo
Katika hatua nyingine Mhandisi Kundo ametoa miezi mitatu kwa kampuni ya simu ya tigo kuhakikisha imefikisha nishati ya umeme katika mnara wa mawasiliano wa kampuni hiyo uliopo katika kijiji cha Mdimba unaotumia nishati ya mwanga wa jua pekee wakati nishati ya umeme imekwishafika kijijini hapo.
Aidha, katika ziara yake wilayani Newala Mhandisi Kundo amefanya ufuatiliaji wa minara ya mawasiliano ya kampuni ya simu ya Halotel iliyopaswa kujengwa kwa ruzuku kutoka Serikalini kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) na kukuta hakuna ujenzi wowote uliofanyika mpaka sasa ukizingatia kuwa mkataba wa ujenzi wa mnara wa Halotel katika kijiji cha Chilangala ulisainiwa toka Januari, 2020 na utekelezaji wake ulikuwa wa miezi 9 lakini hakuna utekelezaji wowote uliofanyika.
Mhandisi Kundo ameiagiza UCSAF kufanya ufuatiliaji wa minara hiyo na kuhakikisha imejengwa vinginevyo fedha zilizotolewa na Serikali kwa ajili ya ujenzi huo zirejeshwe UCSAF na stakabadhi ya kurejesha fedha hizo ziwasilishwe sehemu husika kwa uthibitisho.
Aliongeza kuwa mradi huo una sintofahamu nyingi kwasababu mtandao wa Halotel tayari unapatikana katika eneo husika wakati jukumu la msingi la Mfuko huo ni kufikisha mawasiliano katika maeneo ambayo hayajafikiwa na huduma ya mawasiliano.
Naye Mbunge wa Newala Vijijini Mhe. Maimuna Mtanda ametoa rai kwa watendaji wa Serikali waliopewa dhamana ya kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo hususan miradi ya mawasiliano kuwajibika ipasavyo kwa lengo la kuhakikisha wananchi wanapata huduma yenye kiwango kilichokusudiwa.
Akizungumza katika ziara hiyo Mkuu wa wilaya ya Newala Mhe. Mwangi Kundya amesema kuwa amepokea maelekezo yanayohusu Wilaya na Kamati ya Ulinzi na Usalama na kuahidi yatafanyiwa kazi kwa kuchukua hatua Madhubuti na kwa wakati ili kuhakikisha kero na malalamiko ya wananchi kuhusu mawasiliano yanapatiwa majibu.