Mabingwa wa Soka Ligi ya Wanawake Tanzania Bara Simba Queens leo Jumanne (Julai 13) jioni watacheza mchezo wa kirafiki dhidi ya timu ya Taifa ya Wanawake (Twiga Stars), Uwanja wa Uhuru jijini Dar es salaam.

Simba Queens watautumia mchezo huo kama maandalizi ya kuelekea michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki, ambapo bingwa wake atashiriki moja kwa moja michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika baadae mwaka huu.

Upande wa Twiga Stars nao watautumia mchezo wa kirafiki dhidi ya Simba Queens kama sehemu ya maandalizi yao, baada ya kikosi chao kuitwa kambini na Kocha Mkuu Bakari Nyundo Shime mwishoni mwa mwezi uliopita.

Katika hatua nyingine, baada ya mchezo huo Simba Queens watakabidhiwa Kombe la Ubingwa wa Ligi Kuu ya Wanawake 2020/21 ambao wameshinda kwa mara ya pili mfululizo.

Simba Queens ilitawazwa kuwa Mabingwa wa Ligi Kuu ya Wanawake baada ya kufikisha alama 51 mbele ya Yanga Princes waliomaliza Ligi hiyo wakiwa nafasi ya pili kwa kufikisha alama 50.

Mhandisi Kundo atoa maelekezo kwa watoa huduma kuhusu ulinzi wa minara ya mawasiliano
Hanspope: Waamuzi wa nchi hii ni 'UKAKASI'