Mshambuliaji mpya wa klabu ya Young Africans Michael Sarpong, amekiri uwepo wa ushindani wa kweli katika Ligi Kuu Tanzania Bara, baada ya kucheza Ligi hiyo kwa mara ya kwanza.
Sarpong aliesajiliwa na Young Africans mwezi uliopita baada ya kuachwa na Rayon Sport ya Rwanda, amesema hakutarajia kama Ligi Kuu Tanzania Bara ingekua na ugumu wa namna hiyo, lakini hana budi kupambana na kufikia lengo la kufunga mabao yatakayoisadia klabu yake.
Tayari mshambuliaji huyo ameshaifungia Young Africans bao moja, wakati wa mchezo wa kwanza dhidi ya Tanzania Prisons, ulichezwa Septemba 06 Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es salaam.
Amesema ugumu wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara unatokana na kila timu shiriki kuwa utayari wa kupambana wakati wote, tofauti na ligi nyingine katika ukanda wa Afrika mashariki na kati.
“Ligi ya Tanzania ina ushindani mkubwa, kutokana na kila timu kujipanga kupata matokeo mazuri pindi inapokuwa uwanjani, ninaona jinsi timu zilivyojipanga vizuri kila moja inataka kushika nafasi ya juu,” amesema Sarpong.
Kuhusu mchezo wa mzunguuko wa pili dhidi ya Mbeya City uliomalizika kwa Young Africans kuibuka na ushindi wa bao moja kwa sifuri lililofungwa na beki Lamine Moro, mshambuliaji huyo kutoka nchini Ghana amesema ulikuwa mgumu, lakini ameshukuru timu yake kuondoka na alama tatu muhimu.
Kuhusu ushindani wa nafasi kwenye kikosi cha kwanza cha Young Africans, Sarpong amesema ni mkubwa, lakini atazidi kujituma kwa nguvu zote kila akipata nafasi ili kujihakikishia kucheza na kuipa mafanikio timu kama alivyoahidi kipindi anatua nchini.
“Ninashukuru wachezaji wenzangu wamenionyesha ushirikiano kuanzia nilipofika sijaona tofauti yoyote, ninaahidi mashabiki wangu kufanya vizuri,” amesema.
Katika hatua nyingine amewataka mashabiki na wanachama wa Young Africans kuendelea kumpa ushirikiano ili aweze kuipa mafanikio klabu hiyo pindi watakapokutana na Kagera Sugar, mwishoni mwa juma hili kwenye mchezo wa mzunguuko wa tatu, utakaochezwa Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.