Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), David Silinde amesema michango inayoruhusiwa katika suala la elimu ni uchangiaji wa hiari na hauhusishi wanafunzi kuzuiwa kuhudhuria masomo.
Amesema hayo leo Juni 8, 2021 katika kipindi cha maswali na majibu bungeni, wakati akijibu swali lililoulizwa na mbunge wa Nkasi Kaskazini Aida Khenani alilouliza kwanini serikali inasema elimu ya shule ya msingi na sekondari ni bure wakati wazazi wanaendelea kuchangishwa michango ya elimu?.
“Waraka wa elimu namba 5 ulishazungumza elimu msingi ni elimu bila ada, waraka wa elimu namba 3 wa mwaka 2016, unaeleza wajibu wa serikali na mwananchi ambapo ni pamoja na kushiriki katika miradi ya maendeleo hususan uchangiaji wa hiari na wasilazimishwe,” amesema Silinde.
Naye Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako wakati akichangia hoja ametoa wito kwa wazazi kuona umuhimu wa kushirikiana na serikali kujenga mazingira mazuri ya upatikanaji wa elimu iliyo bora.
“Nitoe wito kwa wazazi kuendelea kuona umuhimu wa kushirikiana na serikali kwa sababu mazingira yanapokuwa mazuri watoto wanakuwa na uhakika wakupata elimu iliyo bora, tunachosisitiza ni marufuku mwanafunzi kufukuzwa shule sababu ya michango,” amesisitiza Silinde.