Aliyewahi kuwa kocha mkuu wa timu ya taifa ya Uganda (The Cranes) Milutin ‘Micho’ Sredojevic ametangazwa kuwa mkuu wa benchi la ufundi la mabingwa wa Afrika mwaka 2012, timu ya taifa ya Zambia (Chipolopolo).
Micho alitangazwa jana kushikwa wadhifa huo, baada ya kusaini mkataba wa miaka miwili na uongozi wa chama cha soka nchini Zambia (FAZ), ambao wanaamini kocha huyo kutoka nchini Serbia atafanikisha malengo ya kufanya vyema kwenye michuano ya Afrika na ile ya dunia.
Viongozi wa soka nchini Zambia kwa muda mrefu walikua wakimsaka kocha wa kudumu wa kikosi chake, huku wakiwa na lengo la kurekebisha makosa ya kuzikosa fainali za afrika (AFCON 2019), baada ya kusitisha mkataba wa Sven Vandenbroeck ambaye kwa sasa ni kocha wa mabingwa wa soka Tanzania bara Simba SC.
Mtihani wa kwanza kwa Micho utakua mpambano wa kuwania kufuzu fainali za Afrika (AFCON 2021) dhidi ya Botwana, ambao utachezwa nyubani na ugenini mwezi ujao.
Kocha Sven Vandenbroeck akiwa na Rais wa chama cha soka Zambia (FAZ) Andrew Ndanga Kamanga baada ya kusaini mkataba wa kukinoa kikosi cha Chipopolo mwaka 2018.
Zambia walianza vibaya harakati za kuwania nafasi ya kushiriki fainali za Afrika (AFCON 2021), kufuatia kupoteza mchezo dhidi ya Algeria kwa kufungwa mabao matano kwa sifuri dhidi ya Algeria, kisha wakaangukia pua mbele ya Zimbabwe kw akufungwa mabao mawili kwa moja, hali inayowafanya kuburuza mkia wa msimamo wa kundi H.
Shabaha nyingine kwa kocha Micho, ni kufanikisha taifa la Zambia linafuzu fainali za kombe la dunia 2022, kwa kuhakikisha wanashinda michezo dhidi ya Tunisia, Mauritania na Equatorial Guinea ili wafanikishe azma ya kucheza hatua ya mtoano na baadaye kukata tiketi ya kuelekea Qatar.
Kocha Micho mwenye umri wa miaka 50, anashika jukumu la kuwa kocha mkuu wa timu ya taifa kwa mara ya tatu, tangu alipoanza kufanya hivyo mwaka 2017 akiwa na Rwanda kisha akatimkia Uganda.
Mwaka huo alifanikiwa kuipeleka Uganda kwenye fainali za mataifa ya Afrika (AFCON 2017) zilizofanyika Gabon, na kumaliza gundu kwa taifa hilo la Afrika mashariki kushindwa kufuzu kwa miaka 39.
Micho alianza shughuli za kufundisha soka barani Afrika mwaka 2001 akiwa na klabu ya SC club Villa ya Uganda, na baadae alitimkia Ethiopia kujiunga na Saint George SC kabla ya kukinoa kikosi cha Orlando Pirates ya Afrika kusini.
Pia aliwahi kupita kwenye klabu za Young Africans ya Tanzania na Al Hilal ya Sudan.