Milio ya risasi imeendelea kusikika jijini Khartoum wakati mapigan kati ya jeshi na wanamgambo nchini Sudan, yakiingia wiki ya 8 na kujeruhi watu kadhaa, ambapo pia watu wanaojitolea wamezika maiti 180 ambazo hazikuweza kutambuliwa.
Tangu kuanza kwa mapigano hayo Aprili 15, 2023 kati ya jeshi linaloongozwa na Jenerali Abdel Fattah al-Burhane, na wanamgambo wa Kikosi cha Msaada wa Haraka cha RFS chini ya Jenerali Mohamed Hamdane Daglo, mashirika ya kutoa misaada ya kibinadamu na watu wanaojitolea, wanasema hakuna urahisi wa kuhifadhi miili kutokana na hali mbaya ya usalama.
Aidha, Shirika la Hilali Nyekundu la Sudan, limesema katika taarifa yake kwamba miili hiyo 180 ambayo haikutambuliwa na imezikwa, 102 ilipqtikana eneo la kusini mwa Khartoum na 78 huko Darfur.
Mzozo huo tayari umegharimu maisha ya zaidi ya watu 1,800 na kufanya zaidi ya watu milioni moja na nusu kuyakimbia makazi yao na wengine 400,000 kukimbilia nchi jirani kuomba hifadhi.