Meneja wa Kikosi cha Arsenal Mikel Arteta amesema “suluhu, siyo tatizo” katika uhusiano wake na mshambuliaji wa zamani wa The Gunners, Pierre-Emerick Aubameyang aliyetua FC Barcelona mwezi Januari.
Aubameyang ambaye alikua hana mahusiano mazuri na Arteta, aliondoka Kaskazini mwa London wakati wa Dirisha Dogo la Usajili, hali ambayo ilizua taharuki kwa baadhi ya mashabiki wa Arsenal ambao walitamani kumuona Mshambuliaji huyo kutoka Gabon akiendelea kuwepo klabuni hapo.
Arteta amelazimika kufunguka kuhusu uhusiano wake na Aubameyang, kufuatia Mshambuliaji huyo kueleza namna alivyoishi na bosi wake katika kipindi chote tangu alipoanza kufanya naye kazi miaka miwili iliopita.
Mshambuliaji huyo alisema “lilikuwa ni tatizo tu na (Arteta)”, wakati alipojiunga na FC Barcelona kwa uhamisho huru mwezi uliopita.”
Arteta amejibu kwa kusema: “Ilikuwa ni suluhu kwa asilimia 100. Ninaweza kutazama machoni mwa kila mtu.”
“Ninafanya mambo mengi kimakosa, kusema kweli lengo kila wakati ni bora na sio kwangu mimi, ni kwa ajili ya timu nzima.
“Ninashukuru sana kwa kile Auba alichokifanya katika klabu na mchango wake tangu alipokuwa hapa. Jinsi ninavyojitazama mimi katika uhusiano ule ni suluhu, siyo tatizo.”
Arteta alithibitisha kuwa mshambuliaji Mfaransa Alexandre Lacazette atakuwa nahodha wa Arsenal hadi mwishoni wa msimu, wakati ambapo mkataba wa nyota huyo mwenye umri wa miaka 30 utakapokaribia kumalizika.
Alipoulizwa kuhusu mchezaji wa kimataifa wa Gabon, Aubameyang kusema yeye alikuwa tatizo. Raia huyo wa Hispania alisema: “Hayo ni maoni yake, hilo ndilo alililosema na unapaswa kuheshimu hilo.”