Meneja wa Kikosi cha Arsenal, Mikel Arteta amesisitiza kuwa, hataruhusu wachezaji wake kupoteza alama kwani anataka kuona wakipambana hadi hatua ya mwisho kuwania ubingwa wa Ligi Kuu ya England licha kupata upinzani mkubwa kutoka kwa Manchester City.
Arsenal juzi Jumanne (Mei 02) ilifanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Chelsea katika London Dabi na kurejea kileleni kwa muda, lakini jana Jumateno (Mei 03) ilirudi nafasi ya pili kufuatia Man City kuibanjua West Ham Utd.
Arsenal imefikisha alama 78 baada ya kucheza Michezo 34, huku Man City ikiwa kileleni ikikusanya alama 79 ikicheza Michezo 33.
Arteta bado anaamini wapo kwenye njia sahihi kwani lolote linaweza kutokea ndiyo maana anataka kuona timu yake ikishinda mechi zote zilizosalia.
“Tumebaki na mechi nne na kwa sasa tupo nyuma ya Man City kwa tofauti ya alama moja. Ni lazima tupambane lolote laweza kutokea, nafasi bado tunayo.”
“Hatuwezi kuacha kirahisi kupambana, tumekuwa juu kwa miezi mingi, tunaendelea kupambana kuhakikisha tunakusanya alama, huwezijua mwisho nini kitatokea.”
“Ndiyo maana katika mchezo wa juzi tulicheza kwa staili tofauti na hii ni katika kupata alama, timu ilikuwa kwenye ubora wake na ninaamini hata mechi zijazo wachezaji wataendelea kuwa bora na kupambana, kwa sasa ushindi ni muhimu kwetu.” amesema Arteta