Kocha Mkuu wa Arsenal, Mikel Arteta amekuwa na hofu kufuatia winga Bukayo Saka, kupata jeraha la misuli katika mchezo wa Kundi B wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya RC Lens ya Ufaransa Juzi Jumanne (Oktoba 03).
Katika mchezo huo ambao Arsenal ilifungwa mabao 2-1, Saka alitolewa dakika ya 34 huku nafasi yake ikichukuliwa na kiungo Fabio Vieira.
Kabla ya kutolewa, Saka alikaa chini uwanjani na kuanza kuugulia maumivu katika miguu yake.
Akizungumza nchini Ufaransa, Arteta alisema hali ya nyota huyo kuugulia maumivu hayo ilimpa hofu, lakini hajutii kumpanga katika mchezo huo.
“Hatujui kitu chochote zaidi, ilikuwa inatosha sana kutomruhusu aendelee kucheza mechi na hiyo ilitupa hofu,” alisema Arteta.
Alipoulizwa kama anajutia kumpanga nyota huyo katika mechi ya juzi, Arteta alisema hajutii kwani awali alikuwa fiti.
Saka mwenye umri wa miaka 22, hivi karibuni amekuwa akishindwa kumaliza mechi kutokana na kupata majeraha.
Nyota huyo, anaripotiwa kuwa katika hatihati ya kukosekana katika mchezo ujao wa Ligi Kuu ya England wakati Arsenal itakapoikaribisha Manchester City katika Uwanja wa Emirates.
Saka ameanza katika mechi 87 mfululizo za Arsenal katika michuano ya Ligi Kuu ya England.