Katibu Mkuu wa Uchukuzi, Gabriel Migire, amesema kuwa Meli mpya ya Mv Mwanza ‘Hapa Kazi Tu’ itainua uchumi na uwekezaji kwenye mikoa nane ya kanda ya ziwa, ni upendeleo wa Serikali kwa wakazi wanaozunguka ziwa hilo nakuwataka kujipanga kuitumia kwa kufanya biashara.

Amesema hayo wakati wa wakati wa hafla ya ushushwaji wa meli hiyo kwenye maji iliyofanyika Bandari ya Mwanza kusini ambapo ameeleza kuwa mikoa inayotarajia kufaidika na ufanyaji kazi wa meli hiyo ni pamoja na; Mwanza, Kagera, Mara, Geita, Tabora, Simiyu, Kigoma na Shinyanga.

“Mkoa wa Mwanza na Mikoa inayoizunguka inapaswa kuanza kujiandaa ili kutumia fursa hii adhimu. Huu ni upendeleo mkubwa ambao umefanywa na serikali kuhakikisha kuwa usafiri katika Ziwa Victoria unaendelea kuimarika,”amesema Migire.

Katibu Mkuu wa Uchukuzi, Gabriel Migire

”Baada ya Meli hii kujengwa tunajukumu la kuhakikisha wale wanaoiendesha wanazingatia miongozo ili kuhakikisha meli hii inadumu kwa muda mrefu,” amesema Migire

Naye Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Adam Malima amesema uwepo wa meli hiyo utachochotea shuguli za kiuchumi kwa wananchi pamoja na miradi mingine inayoendelea mkoani humo ambayo ni ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR, Daraja la JPM (Kigongo-Busisi) na uboreshaji wa uwanja wa ndege wa mkoa huo.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Adam Malima

Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Albert Chalamila amesema usafiri huo utaonganisha mkoa huo na nchi ya Uganda ambao upo jirani yake akidai mizigo yote ya tani 400 itakayobebwa kwenye meli hiyo itatokea mkoani Kagera.

Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigela  amesema kwakuwa wao ni wazalishaji wakubwa wa dhahabu nchini ambapo wanazalisha kati ya asilimia 60 hadi 70 ya dhahabu yote nchini na mzunguko wa fedha kwa wananchi wa mkoa huo ni mkubwa basi meli hiyo itachochea shuguli za kiuchumi na uwekezaji.

Mkuu wa Mkoa wa Mara, Meja Jenerali Suleiman Mungiya Mzee ameipongeza Serikali na kudai wanafarijika kuona inakamilisha miradi iliyoanzishwa na Hayati Dk John Magufuli enzi za uhai wake.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Dk Batilda Buriani amesema mkoa huo ni wazalishaji wakubwa wa zao la tumbaku ambapo wanazalisha asilimia 60 ya tumbaku nchini, wazalishaji wa pamba pamoja na mazao ya chakula ukiwemo mpunga, choroko, karanga pamoja na asali hivyo meli hiyo wataitumia kusafirisha mazao yao wanayozalisha.

“Lakini pia sisi ni wafugaji wa ng’ombe. Tunaongoza kwa kuwa na ng’ombe wengi Tanzania nzima, tuna ng’ombe takribani milioni 2. 7. Sisi tunataka wafugaji wetu wabadilishe koo za ng’ombe hivyo tunategemea kupata ng’ombe kutoka Uganda ambao tutaweza kubadilisha koo na kufuga kisasa zaidi,”amesema Dkt Batlida

Wabunge ni Walafi na Wachoyo: Heche
LIVE: Meli ya MV Mwanza ''Hapa Kazi Tu'' yashushwa majini