Wakati Young Africans wakihusishwa na mpango wa kufanya maboresho ya kikosi chao kuelekea msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara, taarifa zinadai kuwa Mshambuliaji kutoka DR Congo Heritier Makambo huenda akarejea Jangwani kwa dau nono.
Taarifa zinasema kuwa klabu ya Hoyora AS ya Guinea imemuweka sokoni mshambuliaji huyo kwa dau la Shilingi milioni 100, ambazo ni kama fidia ya kuvunja mkataba wa mwaka mmoja uliosalia baina ya pande hizo mbili.
Kwa utaratibu huyo Uongozi wa Young Africans utalazimika kutoa kiasi hicho cha pesa, kama kweli wanahitaji huduma ya Makambo kwa mara nyingine tena, hasa baada ya kufanya mambo makubwa msimu wa 2018/19 akiwa na klabu hiyo kongwe katika ukanda wa Afrika Mashariki na kati.
Makambo tangu aliposajiliwa Horoya AS mwishoni mwa msimu wa mwaka 2018/19 akitokea Young Africans, ameshindwa kutamba kama ilivyokua katika Ligi Kuu Tanzania Bara, hatua ambayo imewapa msukumo viongozi wa klabu hiyo kumuweka sokoni .
Akiwa Young Africans, Makambo aliifungia timu hiyo mabao 17 msimu wa 2018/19 na kumaliza nafasi ya tatu kwenye chati ya wafungaji nyuma ya Meddie Kagere wa Simba na Salim Aiyee wa Mwadui FC waliofunga mabao 23 na 18.
Makambo aliisaidia Young Africans kumaliza nafasi ya pili kwenye msimamo Ligi Kuu msimu wa 2018/19 ikiwa na alama 86, nyuma ya Simba SC waliokuwa Mabingwa kwa kufikisha alama 93.