Licha ya kuendelea kwa tetesi huenda akatemwa mwishoni mwa msimu huu baada ya mkataba wake kufikia kikomo, Kocha Mkuu wa Geita Gold, Fred Felix Minziro amesema bado hafahamu kama ataendelea kuwa kocha wa timu hiyo ama la.

Kocha Minziro amesema mkataba wake unamalizika mwisho wa msimu huu, na ana ofa kutoka timu mbalimbali ingawa hakuweka wazi timu hizo.

Hata hivyo, Minziro amesema anatarajia kukutana na uongozi wa timu hiyo hivi karibuni kufahamu kama ataendelea kuinoa timu hiyo au la.

“Ni kweli namaliza mkataba mwisho wa msimu huu, zimesalia siku chache mno lakini bado hakuna mazungumzo na uongozi kuhusiana na hilo japokuwa natarajia kukutana nao kabla ya kucheza mechi mbili zilizosalia za ligi,” amesema beki huyo wa zamani wa pembeni wa Young Africans

Amesema mpaka sasa anashindwa kufanya usajili au kutoa mapendekezo ya wachezaji wapya kwa ajili ya kuichezea timu hiyo msimu ujao kwa sababu bado hajakutana na uongozi kufahamu hatima yake.

“Kama inavyoonekana kweli tunaelekea kipindi cha usajili, kuisuka vizuri zaidi timu kwa ajili ya msimu ujao lakini huwezi kufanya hivyo kwa sasa sababu bado haijafahamika itakuwaje siku za usoni kuhusu kuendelea kubaki Geita,” amesema Minziro

Dullah Mbabe apeleka ombi Ikulu
Tanzania, Afrika Kusini kushirikiana sekta ya Utamaduni, Sanaa na Michezo