Hatimaye Kiungo Mshambuliaji kutoka nchini Msumbiji Jose Luis Miquissone amemalizana na Uongozi wa Mabingwa wa Soka Barani Afrika Al Ahly, kwa kuvunja mkataba, hali ambayo inamfanya kuwa mchezaji huru katika kipindi hiki cha maandalizi ya msimu mpya 2023/24.

Maamuzi ya kuvunjwa kwa mkataba baina ya pande hizo mbili yamefikiwa, huku Miquissone akihusishwa kurejea Simba SC ambayo alikuwa akiitumikia kabla ya kutimkia Misri miaka miwili iliyopita.

Kampuni ya Uwakala ya Brand Arc Sports inayomsimamia Miquissone imethibitisha kuvunjwa kwa mkataba huo, huku ikiahidi kutoa taarifa zaidi kuhusu mipango ya baadae ya mchezaji huyo siku kadhaa zijazo.

Taarifa iliyothibitishwa kuvunjwa kwa mkataba baina ya Uongozi wa Al Ahly na Luis Miquissone ambayo imesambazwa katika mitandao ya kijamii inasoneka kama ifuatavyo.

Kama wakala anayewakilisha mchezaji wa kimataifa wa Msumbiji Luis Miquissone, tungependa kuthibitisha kuvunjwa kwa mkataba baina ya uongozi wa Al Ahly na mchezaji wetu.

Uamuzi huo umefikiwa kwa furaha baada ya winga huyo kumaliza mkataba wake wa mkopo na klabu ya Abha ambayo inashiriki Ligi Kuu ya soka nchini Saudi Arabia ‘Saudi Arabia Pro’.

Luis alijiunga na Ahly, ambao ni wababe wa Misri na Klabu ya Karne, miaka miwili iliyopita, na amefanikiwa kucheza katika baadhi ya nchi za Afrika akianzia nyumbani Msumbiji, Afrika Kusini na Tanzania na baadae Saudi Arabia.

Sasa anatarajia kupata changamoto mpya mahala pengine, ambapo Brand Arc Sports inaahidi kuwajuza mashabiki wake taarifa zaidi wapi atakapocheza msimu ujao.

“Ningependa kumshukuru Mwenyekiti wa klabu, uongozi, wachezaji wenzangu na makocha ambao nimefanya nao kazi na wakati wangu wote hapa. Pia nitoe shukrani zangu kwa mashabiki wa klabu hii kubwa ya Al Ahly,” alisema Luis.

Mwenyekiti wa Kampuni Brand Arc, Thato Matuka, ambaye alifanikisha mpango wa mchezaji huyo kujiunga na Al Ahly na sasa kuvunjwa kwa mkataba wake amesema: “Tunaishukuru klabu kwa nafasi hiyo. Hatujutii chochote, Luis alipambana kwa ubora wake katika klabu. Tunafunga ukurasa huu na tunaendelea kupata maombi mbalimbali na tutawajuza mustakabali Luis, tuna imani katika mwelekeo uliopo na tutafanikiwa,”

Hofu ya usalama: Shule zafungwa kwa muda usiojulikana
Polisi watoa ufafanua tukio kifo cha Mtumishi Kilosa