Simba SC inaendelea kujifua mazoezini kabla ya kuanza safari kwenda mjini Ndola nchini Zambia tayari kwa mchezo wa Mkondo wa kwanza wa Mzunguuko wa pili wa Ligi ya Mabingwa Afrika, huku wachezaji wapya wa timu hiyo, Luis Miquissone na Aubin Kramo wakipangua kikosi kwa kumpa kocha Roberto Oliveira ‘Robertinho’ mfumo mpya kwa sasa.
Kramo amerejea kutoka kuwa majeruhi na ameanza kuwasha moto akiwa sambamba na Miquissone ambaye tangu arejee kikosini alionekana mzito, lakini kwa sasa yupo fiti na kumpagawisha Mbrazili huyo ambaye amekiri kwa sasa ana machaguo mengi atakayotumia kwenye mechi ya ugenini na nyingine zilizopo mbele yake.
Robertinho amesema kuwaka kwa wachezaji hao wawili na kuibuka kwa vita ya kuwania namba kwa washambuliaji Moses Phiri, Willy Esomba Onana na Jean Baleke, kunamfanya sasa wajipange kwani kila mmoja ana nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza, muhimu ni timu kupata matokeo mazuri uwanjani.
Robertinho amefunguka hayo baada ya kuwatumia mastaa hao kwenye mchezo mmoja wa kirafiki dhidi ya Cosmopolitan na kushinda mabao 5-l huku washambuliaji hao wakitupia kila mmoja bao moja.
Kocha huyo ambaye ni muumini wa kutumia mfumo wa 4-2-3-1, 4-1-3-2 na mara nyingine akitumia 4-1-3-1-1 amesema kwa sasa atalazimika kubadili mfumo kutokana na aina ya mechi zilizo mbele yake huku akikiri kuwa wachezaji wake wapo katika nafasi nzuri ya kucheza.
Mfumo wa 4-2-3-l amekuwa akitumia mabeki wanne, viungo wawili wa chini viungo washambuliaji wawili mmoja wa juu na mawinga wawili na wamekuwa wakitumika Clatous Chama, Said Ntibazonkiza na Kibu Denis na mshambuliaji mmoja ambaye ni kati ya Baleke ama Phiri.
4-1-3-2 hapa anatumia mabeki wanne, kiungo mmoja mkabaji ambaye ni kati ya Sadio Kanoute, Fabrice Ngoma au Mzamiru Yassin, viungo washambuliaji watatu na washambuliaji wawili ambao ni chaguo lake mwenyewe kana alivyosema kuwa safu yake ya ushambuliaji ni imara.
Robertinho amesema kutokana na wachezaji kuanza kuongeza utimamu wa mwili tofauti na walivyoanza msimu huu, anaona kuna kila sababu ya kubadili mfumo wake wa uchezaji kulingana na mechi husika.
Ameongeza, ili mchezaji apate nafasi ya kucheza ni lazima amuonyeshe katika mazoezi yake kwa kuhakikisha anatimiza majukumu yote ya ndani ya uwanja atakayompa.
“Wachezaji wangu wote kwa asilimia kubwa nimewatumia kwenye mechi mbili za kirafiki tulizocheza wameonyesha wana kitu wanaweza kukifanya ndani ya timu mfano Aubin Kramo na Luis Miquissone wameonyesha kuimaraika zaidi.
“Kutokana na mabadiliko ya uchezaji wao wananifikirisha kuwa na mifumo tofauti na nilivyozoeleka na itakuwa inabadilika kutokana na mechi husika.
Kuhusu ubora wa wachezaji kila mmoja amekuwa na umuhimu wake kulingana na mechi husika.” amesema kocha huyo aliyetua Januari mwaka huu kutoka Vipers ya Uganda.
Akizungumzia kutumia washambuliaji watatu kwenye mchezo mmoja ambao ni Onana, Phiri na Baleke amesema amegundua kitu kutoka kwao akiweka wazi kuwa akifanya hivyo ana uhakika wa kupata mfungaji bora kutoka katika nyota wake hao ambao amekiri kuwa kila mmoja anakuwa na kiu ya kufunga.
“Baleke, Onana na Phiri wote ni wachezaji wazuri kwenye umaliziaji na kila mmoja ana kiu ya kufunga hivyo naweza kutengeneza pacha nzuri na yenye faida kwa timu hasa kwenye suala la ushindani wa kupachika mabao mengi,” amesema Robertinho na kuongeza;
“Lakini wakati watatu hao wakifanya vizuri ameingia kati Kramo pia amekuwa mchezaji ambaye anajituma sana ameongeza chachu ya ushindani kwenye kikosi changu, nafurahia kuwa na wachezaji wenye malengo yanayofanana naamini sasa kila nitakayempa nafasi atanipa matokeo chanya”