Siku zote binadamu hukumbukwa kwa kile alicho kifanya na kuna wakati pia binadamu huzidi kutambulika kwa yale anayoyafanya, Hata kwa upande wa soka pia hali hii ipo hivyo hivyo ambapo mchezaji huweza kutambulika zaidi kwa kuiletea mafanikio timu yake au kwa kufanya jambo lolote ambalo linaweza kuteka hisia za mashabiki wa mchezo huo.
June 23 mwaka huu kwenye michuano ya AFCON kulikuwa na mechi baina ya Taifa Stars na Senegal ambapo Stars ililala kwa mabao 2-0 na baada ya mchezo huo ambao ulipigwa kwenye dimba la 30 june Stadium huku ushindi huo wa Simba wa Teranga ulichagizwa na mabao ya Keita Balde na Krepin Diatta.
Baada ya mchezo huo Krepin Diatta mbali na kufunga goli la aina yake kwa shuti kali lililomuacha kinywa wazi mlinda mlango wa Taifa Stars, Aish Manula na kuihakikishia ushindi timu yake lakini pia Diatta aliibuka mchezaji bora wa mchezo na baada ya hapo watu mbalimbali wakaanza kumzungumzia katika kila kila kona hususani kwenye mitandao ya kijamii.
Dar24 Media ikaona si vyema kuliacha suala hili likapita tu pasi na watu kutokujua walau kwa uchache kuhusu historia ya maisha ya soka ya mchezaji Krepin Diatta kwa ujumla.
Krepin Santos Diatta ni kiungo wa kushoto wa ambaye ni raia wa Senegali aliyezaliwa 25 february 1999 ambapo hadi hivi sasa ana miaka 20 ana urefu wa futi 5 na inchi 8, uzito wa kilo 68 zinazomfanya kuwa mnyumbulifu na kusababisha usumbufu mkubwa kwa mabeki huku silaha yake kubwa ikiwa ni mguu wake wa kulia anaoutumia vyema katika nafasi ya kiungo upande wa kushoto anapokuwa uwanjani.
Maisha ya mchezaji huyo kwa upande wa soka yalianzia katika akademi ya Oslo nchini Norway na baadaye alijiunga na timu ya Sarpsborg aliyodumu nayo kwa mwaka mmoja akiichezea michezo 22 na kufunga mabao 3
Huenda huo ulikuwa mwanzo mzuri wa maisha ya soka ya mwanaume huyo ambaye wadau wengi wa soka hapa Tanzania wamekuwa wakidaiwa kumuita mwamba ambapo januari 2018 alijiunga na Club Brugge ya Ubelgiji kwa mkataba mrefu mpaka mwaka 2022 kwa dau la Euro 2m ambapo anacheza nafasi ya ushambuliaji ndani ya Club hiyo.
Mwaka 2017, akiwa na umri wa miaka 18, Krepin Diatta alianza kumendewa na vilabu vikubwa barani Ulaya ambapo kupitia tovuti ya Manchester Evening iliripoti kijana huyo kwamba anahitajika na Manchester United na mwenyewe alikiri kufanya nao mazungumzo zaidi ya mara kadhaa ambapo aliyekuwa kocha wa Manchester united kwa wakati huo, Jose Mourinho aliwaagiza wasaidizi wake kumfuatilia mchezaji huyo japo dili halikukamilika.
Wakati huo kinda huyo alikuwa akiitumikia klabu ya Sarpsborg 08 ya Norway, na United waliamini wangeweza kuangalia uwezo wake baada ya mchezo dhidi ya timu ya Odds Ballklubb ambapo timu ya kina Diatta ilikua ikijiandaa na mchezo dhidi ya timu hiyo.
Nyota huyo aliyebarikiwa kipaji cha kutumia vizuri mipira iliyokufa alifanya mazungumzo na masakuti zaidi ya mara mbili na United baada ya kumalizika kwa michuano ya kombe la dunia kwa vijana chini ya umri wa miaka 20 aliyowahi kushiriki kwa wakati huo akiwa na miaka 18 ambapo aliwahi kukiambia chombo cha habari cha TV2 kuwa ameshafanya mazungumzo na maskauti wa United zaidi ya mara mbili.
Nikimnukuu Diatta kuhusiana na mpango wa kwenda Manchester United alisema “Sikufahamu kuwa Manchester United wananifuatilia, lakini kujiunga nayo ni ndoto ambazo zitakuja kutimia. Nafikiri niko vizuri, tutafahamu hapo baadaye nini kitakuja kutokea.”
Siku zote kila kilicho bora huandaliwa vyema ili kiweze kuwa na manufaa siku za usoni na Ubora wa Diatta haukuandaliwa kipindi ambacho Simba wa Teranga au timu ya taifa ya Senegal wakati inajiandaa na AFCON la hasha bali ni kutokana katika akademi za mpira alizopitia,timu za vijana alizocheza.
Pia ubora wake unachagizwa na timu yake ya Club Brugge ya nchini Ubeligiji ambayo anasakata kabumbu timu ambayo ilimaliza nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi kuu nchini humo Ligi ambayo ina jumla ya klabu 16 huku nafasi ya kwanza ikichukuliwa na KRC Genk ya Mbwana Samatta ambayo ni mabingwa wa ligi.
Kila ukionacho ulimwenguni hakikosi rekodi na hata timu yetu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars ina rekodi yake ambayo moja wapo ni kushiriki michuano ya AFCON kwa mara nyingine tena baada ya miaka 39 kupita lakini kwa upande wa Diatta ana rekodi ya kucheza michezo 59 katika ngazi ya vilabu na kufunga magoli matano.
Kijana huyu wa Senegal mara ya kwanza aliitwa kwenye timu ya taifa ya vijana mwaka 2016 na kufanikiwa kuichezea michezo 19 na kufunga mabao 7 ambapo aliisaidia timu hiyo kumaliza nafasi ya pili katika michuano ya Afcon ya vijana ambayo ilipigwa kwenye ardhi ya wana Chipolopolo ya nchini Zambia.
February mwaka huu kinywa cha kocha mkuu wa Senegal Aliou Cise kilitamka jina la Krepin Diatta na kumuorodhesha kwenye orodha ya majina ya wachezaji wa kikosi cha taifa hilo ambacho kinashiriki AFCON katika ardhi ya mafarao nchini Misri.
Mchezo dhidi ya Tanzania ulikua ni mchezo wa pili wa kinda huyo na alifanikiwa kufunga goli moja na kutwaa tuzo ya mchezaji bora wa mechi hiyo.
Kupitia maisha ya soka ya kijana huyu mwenye umri wa miaka 20 tu, viongozi wa soka letu la Tanzania wanatakiwa kujifunza kulisimamia vyema suala la ukuzaji wa vipaji pamoja na kulitekeleza kwa vitendo suala la kutengeneza akademi za mpira za vjina wetu kama kweli tunahitaji mafanikio ya kweli kwenye soka.