Rais John Magufuli na Yoweri Museveni wa Uganda, kwa pamoja wamemtaka Mkandarasi anayejenga bomba la mafuta kutoka Hoima Nchini Uganda mpaka Jijini Tanga kuanza ujenzi mara moja na kuacha kutoa visingizio visivyokuwa na sababu za msingi.
Hayo waliyasema Ikulu jijini Dar es salaam walipokuwa wakizungumza na waandishi wa habari, baada ya wawili hao kumaliza mazungumzo mbalimbali yaliyokuwa yanahusu ushirikiano na maendeleo.
“Ujenzi wa Bomba la Mafuta ulitakiwa na kuanza juzi lakini umeshindikana sijui kwanini, sasa mkandarasi huyo asilete kisingizio tena, ujenzi uanze mara moja,”amesema Rais Magufuli.
Kwa upande wake Rais Museveni ameunga mkono kuharakishwa kwa ujenzi wa bomba kwani mara baada kukamilika kutaziletea faida nchi hizo mbili.
Hata hivyo, ujenzi wa Bomba hilo lenye urefu wa kilomita 1,410, litakalokuwa likisafirisha mafuta ghafi kutoka Ziwa Albert nchini Uganda hadi Bandari ya Tanga linatarajiwa kukamilika, juni 2020 na mradi huo unajengwa na Kampuni ya Total.