Katika kuhakikisha wanaunga mkono juhudi za kupambana na uhalifu wa dawa za kulevya, Shirika la Posta Tanzania (TPC), linasimika mfumo wa kisasa utakaogharimu Sh. Milioni 200 wa kudhibiti usalama na kurahisisha utambuzi wa vitu na matukio hatarishi na haramu yanayopitishwa au kujitokeza kupitia mtandao wa shirika hilo.

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa shirika hilo, Dkt. Harun Kondo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam. amesema kuwa mfumo huo unajumuisha ufungaji wa kamera za kiusalama (CCTV), Posta Kuu ya Dar es Salaam, na tayari mzabuni amesimika mtambo na ataukabidhi kwa shirika wiki ijayo.

“Tumesimika mifumo ya kisasa ya kiusalama, ikiwa ni pamoja na mashine za ukaguzi wa mizigo katika ofisi zenye uwezekano wa kuwa uchochoro wa uhalifu wa aina hii, ikiwa ni pamoja na ofisi za Zanzibar, Kigoma, Dar es Salaam na Arusha,” amesema Kondo.

Aidha, amesema hatua hizo zimechukuliwa na shirika ili kuhakikisha linashiriki na kuchangia kikamilifu jitihada za Serikali ya Awamu ya Tano za kupambana na uhalifu, ikiwa ni pamoja na usafirishaji, uuzaji, utumiaji wa dawa za kulevya, utakatishaji wa fedha haramu, ugaidi, udaganyifu katika utambulisho pamoja na uhalifu mwingine wa kimtandao wa kitaifa na kimataifa.

Mwenyekiti huyo amesema Bodi ya Wakurugenzi ya shirika imedhamiria kuongeza msukumo wa kasi ya usimamizi ili kupambana na uhalifu huo ambao una madhara makubwa kwa jamii.

Hata hivyo, Shirika hilo kwa kushirikiana na vyombo vingine vya usimamizi wa sheria, kwa hivi sasa limeimarisha uhakiki wa mifumo yake na pia ukaguzi wa barua, vifurushi, vipeto na mizigo ili kujiridhisha juu ya usalama na uzingatiaji wa sheria

Makonda aomba viongozi wa dini kuendeleza kuamrisha mema, aombewa dua
Mkandarasi wa bomba la mafuta awachefua JPM, Museveni