Kiongozi wa Muungano wa Azimio la Umoja One Kenya, Raila Odinga, amesema hataki kumegewa nusu mkate na serikali ya Kenya Kwanza akidai umeoza, na kwamba hakuonekana kwenye maandamano kwakuwa alikuwa amelazwa hospitalini baada ya kuugua homa kali.
Odinga ameyasema hayo wakati akihojioa na Taifa Leo akisema aliambukizwa homa kali siku chache zilizopita na ndipo hakuonekana hadharani na kwamba kutokuwepo kwake hakujaathiri maandamano na hiyo ni ishara kwamba Wakenya wamejitolea kupinga ongezeko la ushuru.
“Ninataka Wakenya wajue kwamba, maandamano si ya Baba, Martha Karua wala Kalonzo Musyoka. Yanahusu wote wanaopinga gharama ya juu ya maisha na ushuru wa kupita kiasi. Yanahusu Wakenya wanaotaabika kwa sababu ya yale yanayofanyikia. Hii ndiyo sababu raia wako barabarani,” alisema Odinga.
Kuhusu kauli ya Rais William Ruto ya kutaka mazungumzo, Raila amesema “hakuna haja kukaa naye kwa mashauriano kwa sababu hawezi kutimiza ahadi zake. Hawezi kuaminika, leo atasema hivi kesho anasema vingine. Kenya Kwanza ilitulazimisha kuenda barabarani kwa sababu walikataa matakwa yetu matano wakati wa mashauriano ambayo yalitibuka. Wao ndio wa kulaumiwa.”