Grace Mugabe, mke wa Rais wa zamani wa Zimbabwe, Robert Mugabe ameweka wazi kuwa yeye ndiye aliyemshawishi mumewe ajiuzulu nafasi hiyo kwani alikuwa amekataa.
Grace amewaambia waandishi wa habari kuwa Mugabe aliweka msimamo kuwa hatajiuzulu urais kutokana na kuchukizwa na utaratibu uliotumika kumuondoa ambao yeye anadai ni mapinduzi ya kijeshi.
“Ni mimi ndiye niliyemsihi ajiuzulu,” alisema mama Mugabe. “Baba hakutaka kuweka kalamu kwenye karatasi, ukweli ni kwamba mimi ndiye niliyemsihi ajiuzulu ili kuiweka nchi katika amani,” anakaririwa na NewDay.
Mugabe pia alithibitisha kuwa ni mkewe ndiye aliyemshawishi kujiuzulu lakini yeye alikuwa na msimamo kuwa kila kilichokuwa kinafanyika kilikuwa kinyume cha katiba.
Mama Grace alieleza kuwa Mugabe alikuwa tayari kung’olewa kwa kutumia kura ya kutokuwa na imani naye ambayo ingepigwa na wabunge wa chama chake cha Zanu-PF.
Mrithi wake, Emmerson Mnangagwa amekuwa akikanusha kuwa Mugabe aliondolewa kwa nguvu ya jeshi. Mugabe ameita Mnangagwa kuwa ‘mwanaye aliyemkaidi’.