Waendesha mashtaka nchini Rwanda leo Juni 17, 2021 wameiomba Mahakama ya juu nchini humo kumhukumu kifungo cha maisha jela mkosoaji mkuu wa serikali ya Rwanda, Paul Rusesabagina, kwa tuhuma za ugaidi.
Kwa mujibu wa Sauti ya Amerika (VOA) mjini Kigali waendesha mashtaka wanamshtumu Rusesabagina kwa makosa tisa, ikiwemo kuunda na kufadhili kundi haramu ambalo liliendesha mashambulizi ya kigaidi nchini humo kati ya mwaka 2018/19 na kusababisha vifo vya watu wengi.
Hata hivyo Rusesabagina hakuwepo mahakamani wakati wa kusikilizwa kesi dhidi yake na watuhumiwa wenzake 21.
Amekuwa akisusia kufika Mahakamani akidai kwamba Mahakama za Rwanda hazina mamlaka ya kumfuatilia kwa sababu ya uraia wake wa Ubelgiji, na kueleza kuwa mfumo wa sheria wa nchi hiyo hauwezi kumtendea haki kwa sababu hauko huru.
Rusesabagina, alipata umaarufu kutokana na filamu ya ‘Hotel Rwanda’ ya Hollywood kuhusu mauaji ya kimbari ya Rwanda, filamu hiyo ilikuwa inaelezea juhudi za Rusesabagina katika kuokoa maisha ya maelfu ya raia kutoka jamii ya wa Tutsi wakati wa mauaji ya kimbari ya 1994.
.