Mkurugenzi wa Halmashauri ya Itigi, Pius Luhende amezungumzia tuhuma zinazomkabili za mauaji ya Isaka Petro aliyepigwa risasi akiwa katika kanisa la Wasabato katika kijiji cha Kazikazi mkoani Singida.
Luhende ambaye hivi sasa anapatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida amesema kuwa hahusiki na mauaji hayo akitoa kauli moja tu kuwa “wanampakazia.”
Mkurugenzi huyo ni mmoja kati ya watuhumiwa saba wa mauaji hayo wanaoshikiliwa na Jeshi la Polisi wakihusishwa na tukio hilo lililotokea Jumanne wiki hii.
Ripoti za awali kuhusu tukio hilo zimeeleza kuwa Luhende akiwa na askari wa wanyama pori waliingia ndani ya kanisa hilo wakiwatafuta watu waliokuwa wanatuhumiwa kuharibu mali ya Rose Andrew lililokuwa ndani ya shamba linalomilikiwa na Kampuni ya Tanganyika Packers, na baada ya vurugu Petro alipigwa risasi na kupoteza maisha.
Taarifa ya jeshi la polisi imeeleza kuwa Luhende hakumpiga risasi Petro kwani risasi iliyompata ilifyatuliwa wakati yeye akiwa ameshatoka nje ya kanisa hilo. Hata hivyo, baadhi ya watu waliokuwa ndani ya kanisa hilo wamekuwa na maelezo yanayokinzana na taarifa hiyo ya polisi.
Luhende alilazwa hospitalini ambapo kwa mujibu wa Mwananchi, madaktari wake wameeleza kuwa anasumbuliwa na tatizo la kifua kubana pamoja na moyo.
Akizungumzia maendeleo ya afya yake Daktari anayemhudumia, Dkt. Kuzenza alisema kuwa afya yake inaendelea vizuri kwa kulinganisha na ilivyokuwa awali.
“Tulipompokea alikuwa na hali ngumu kutokana na kubanwa mara kwa mara na kifua. Kwa upande wa mapigo ya moyo tatizo hilo lilianza kupungua. Kwa sasa tumelidhibiti kiasi cha kutosha. Tukijiridhisha kuwa hali yake imeimarika tutamruhusu kuondoka,” alisema Dkt Kuzenza.
Jeshi la polisi mkoani Singida limesema kuwa upelelezi wa tukio hilo la mauaji unaendelea.