Rais Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ameyataka Mataifa yenye rasilimali kuwa na uwazi kwenye uwekezaji na kuweka hadharani kumbukumbu za uzalishaji wao zinazoonyesha mchango stahiki wanaochangia jamii na pato la taifa.

Rais Samia ameyasema hayo wakati akihutubia kwa njia ya mtandao mkutano wa kimataifa wa Taasisi ya Uwazi na Uwajibikaji katika Sekta ya Madini, Mafuta na Gesi Asilia – EITI, uliofanyika Jijini Dakar, Senegal na kudhaminiwa na Rais Macky Sall wa Senegal, Bodi ya EITI na wadau.

Katika hotuba yake fupi aliyowasilisha mbele ya washiriki zaidi ya 1,500 toka nchi zaidi ya 90, Rais Samia amewataka wavunaji wa rasilimali za madini kuhakikisha uwekezaji wao unawanufaisha wananchi wanaoishi katika maeneo husika.

Kwa sasa nchi 57 duniani ni wanachama hai wa EITI, huku Tanzania ikiwa miongoni mwao kupitia taasisi ya TEITI ambapo ujumbe wa Tanzania uliowakilisha Taifa kwenye Mkutano huo, uliongozwa na Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa.

Wajumbe sita walioambatana na Naibu Waziri ni Kamishna wa Madini, Dkt. Abdulrahaman Mwanga, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Danstan Kitandula na Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Jesica Kishoa.

Wengine ni Kaimu Mtendaji wa TEITI, Bi Mariam Mgaya, Mwenyekiti wa Kamati ya TEITI, Ludovic Utouh na Mjumbe wa Kamati ya TEITI, Adam Anthony.

Serikali kuongeza ushuru wa Mafuta, Barabara
Mbwana Makata: Nina deni kubwa Ruvu Shooting