Mkuu wa Mkoa wa Tanga Adam Malima amesema alishirikiana na Uongozi wa Coastal Union kufanikisha mpango wa timu hiyo kucheza Fainali ya Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’ msimu huu 2021/22.
Coastal Union imejihakikishia kucheza Fainali ya michuano hiyo leo Jumapili (Mei 29), baada ya kuichapa Azam FC kwa changamoto ya mikwaju ya Penati 6 kwa 5, katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.
Malima ambaye aliongozana na Mashabiki wa Ciastal Union hadi jijini Arusha kwa ajili ya kuipa nguvu Coastal Union, amesema mpango huo na viongozi ulikuja baada ya kuona kuna nafasi finyu ya kumaliza nafasi ya kwanza ama ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu, hivyo nafasi pekee waliiona ipo ‘ASFC’.
“Nilikaa na viongozi wa Coastal Union tukakubaliana kwa sababu huku kwenye Kombe la Shirikiaho kuna nafasi kubwa ya kwenda kucheza Kimataifa, ukiangalia kwenye ligi wale wawili (Simba na Young Africans) wamejitengenezea utawala wao katika nafasi mbili za juu.”
“Baada ya kufika Nusu Fainali tukaona kwa nini tusicheze Fainali?, Tulijipanga vizuri na ndio maana mmeona tumekuja hapa Arusha na Mashabiki wengi, tunashukuru mungu tumefanikiwa.”
“Tutacheza Fainali hapa Arusha na Young Africans, tutahakikisha tunapambana vyema ili kufanikisha lengo la kucheza kimataifa, tupo vizuri na hatutanii.” amesema Malima.
Young Africans ilitangulia Fainali jana Jumamosi (Mei 28), kwa kuifunga Simba SC 1-0 jijini Mwanza Uwanja wa CCM Kirumba.
Mchezo wa Fainali utapigwa Julai 02 katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid ambao leo Jumapili (Mei 29) umetumika kwa mchezo wa Nusu Fainali.