Mamlaka za Usalama Nchini Ufaransa, zimemtia nguvuni na kumshitaki aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Kibuye nchini Rwanda, Pierre Kayondo kwa tuhuma za kuhusika na mauaji ya kimbari mwaka 1994.
Taarifa za mamlaka hizo zinaeleza kuwa Mkuu huyo wa Mkoa na pia Mbunge wa zamani, alikamatwa na kushitakiwa hapo hapo kwa kushiriki kwenye mauaji hayo ya maangamizi na uhalifu dhidi ya ubinaadamu, ambapo tangu septemba 19, 2023 amehifadhiwa katika mahabusu.
Kayondo, alikuwa akichunguzwa na Ufaransa tangu mwaka 2021, baada ya Jumuiya moja ya wahanga wa mauaji hayo kufunguwa mashitaka dhidi yake ikiaminika kwamba alikuwa akiishi kwenye mji wa kaskazini mwa Ufaransa wa Le Havre.
Hata hivyo, Ufaransa imekuwa kimbilio kubwa la watuhumiwa wanaokwepa kukamatwa kwa ushiriki wao kwenye mauaji ya zaidi ya watu laki nane, wengi wao kutoka jamii ya Watutsi waliouawa ndani ya kipindi cha siku 100 pekee nchini Rwanda.