Kocha Mkuu wa Ruvu Shooting, Charles Boniface Mkwasa amesema hafurahishwi na jinsi kikosi chake kisivyo na muendelezo mzuri wa ushindi kwenye Ligi Kuu na atayatumia mapumziko mafupi ya ligi kufanya marekebisho kwa matatizo yote yanayosababisha jambo hilo ili wakirejea wawe katika kiwango bora.
Mkwasa ambaye alikua kocha msaidizi wa Young Africans msimu uliopita, amesema wachezaji wake wamekua wakicheza tofauti na matarajio yake, hivyo atahakikisha ligi itakaporejea hali ya ushindani kikosini kwake inaimarika na kuonesha umahiri mkubwa dhidi ya timu watakazokutana nazo hadi mwishoni mwa msimu huu.
Amesema wachezjaiw ake wamekua hawana muendelezo mzuri, kama ilivyokua mwanzoni mwa msimu huu, ambapo walionesha soka safi na kufanikiwa kuzinfunga timu kadhaa wakiwemo mabingwa watetezi Simba SC.
“Kweli hatuna muendelezo mzuri kwenye ligi kwa sasa kwa sababu kuna muda tunashinda mechi moja halafu mbili zinazofuata tunapoteza jambo ambalo halifurahishi.
“Kipindi hiki cha mapumziko mafupi ya ligi tunatakiwa kuangalia wapi tunakosea ili kurekebisha na ligi ikirejea turudi kwenye ubora wetu kwa kuhakikisha tunashinda mechi zetu nyingi zilizobaki ili tumalize katika nafasi nne za juu,” amesema Mkwasa.
“Sasa hivi kuna timu zinazopamba kujiokoa na janga la kushuka daraja, kuna zinazowania ubingwa na nafasi za juu hivyo imeifanya ligi kuwa ngumu sana na ili ushinde inatakiwa upambane hasa ,” amesema Mkwasa.
Hadi Ligi Kuu Tanzania Bara inasimama kupisha michezo ya kimataifa, timu ya Ruvu Shooting ilikua inashika nafasi ya sita ikiwa na alama 34, kwenye msimamo wa ligi hiyo ikitanguliwa na klabu za KMC FC, Biashara United Mara, Azam FC, Simba SC na Young Africans.