Kocha msaidizi wa Young Africans Charles Boniface Mkwasa amesema wachezaji wake hawana utimamu wa mwili (hawako fit), ukilinganisha na walivyoonekana wapinzani wao KMC FC, katika mchezo wa wa kirafiki uliopigwa jana Uwanja wa Uhuru. Dar es salaam.
Katika mchezo huo Young Africans walikubali kupoteza kwa kufungwa mabao matatu kwa sifuri, huku wakionyesha kiwango duni mbele ya mashabiki wao waliofika kwa wingi uwanjani hapo.
Mkwasa amesema ni dhahir walistahili kupoteza mchezo huo, kutokana na makosa mengi aliyoyaona kwa wachezaji wake, ambao walianza maandalizi ya kuendelea na ligi kuu, majuma mawili yaliyopita.
“Ni kweli tumepoteza mchezo, ukiangalia ni makosa yetu sisi wenyewe yaliyopelekea tuadhibiwe. Mchezo huu umetusaidia kubaini mapungufu yetu na tutayafanyia kazi kabla ya ligi kurejea,” amesema
“Niwapongeze wenzetu pamoja na kuwa wamefanya mazoezi kwa muda mrefu ukilinganisha na sisi ambao tumefanya mazoezi kwa wiki moja tu. Tunahitaji kuongeza nguvu pamoja na mazoezi mengine”
Young Africans hawakuwa na mchezo mzuri kabisa jana, safu ya ulinzi wakifanya makosa mengi huku safu ya ushambuliaji ikishindwa kufurukuta mbele ya walinzi wa KMC FC.
Mapengo ya wachezaji Bernard Morrison, Papy Tshihimbi na Lamine Moro ambao hawakuwa sehemu ya kikosi kilichoikabili KMC FC yalionekana dhahiri.
Mkwasa aliwaweka nje Morrison na Moro ili kuwaepusha na majeraha zaidi kabla ya mchezo dhidi ya Mwadui FC, utakaochezwa mwishoni mwa juma hili kwenye uwanja wa CCM Kambarage mjini Shinyanga.
Wachezaji hao walipata majeraha madogo kwenye mazoezi ya Young Africans yanayoendelea katika uwanja wa Chuo Cha Sheria, jijini Dar es salaam.