Abiria waliokuwa wakisafiri kwa ndege aina ya Bombardier Q400 ya Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) kutoka Mwanza kuelekea Dar es salaam, walipata hofu baada ya ndege yao kuruka na muda mfupi baadae kulazimika kutua tena katika Uwanja wa Ndege wa Mwanza
Tukio hilo lilitokea jana saa 2.20 asubuhi uwanjani hapo, baada ya ndege hiyo kuruka kisha ikatua ndani ya dakika 20
Wakati ndege hiyo ikitua, Rubani aliwataarifu abiria kuwa wanalazimika kurejea uwanjani hapo kutokana na dharura iliyojitokeza
Aidha, baadhi ya watumishi wa uwanja huo wamesema walishangazwa kuona ndege hiyo ikirejea muda mfupi baada ya kuruka, hali ambayo hutokea pindi ndege inapokuwa na hitilafu ya kiufundi
“Unajua ndege nyingi huanguka wakati wa kuruka na kutua, ndiyo maana jambo hili lilitisha abiria hata wafanyakazi,lakini hakukuwa hitilafu kubwa ya hatari kwani baada ya kurejea na kukaguliwa, ilionekana mlango wa mizigo ya ndege hiyo haukufungwa vizuri, hivyo kuwasha taa ya tahadhari na Rubani kuamua kutua kwa dharura”amesema mmoja wa watumishi hao.
Akielezea tukio hilo, mmoja wa abiria waliokuwa uwanjani hapo aliyekuwa akitarajitarajia kusafiri na ndege nyingine, amesema kuwa wakati ndege hiyo inatua kwa dharura, wafanyakazi wa uwanja huo walionekana kuwa bize kiasi cha kuwashtua wasafiri waliokuwepo uwanjani hapo.
Kwa upande wake Meneja wa Uwanja wa Ndege wa Mwanza Easter Madale, amekiri kuwapo kwa tukio hilo la mlango ingawa amesema hakujua sababu zake.
“Tukio hilo lipo, lakini siwezi kulizungumzia kwa sababu linawahusu watu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege,Kwa hivyo nakuomba uwatafute hao kwasababu ndio wanaojua, ingawa linaonekana halikuwa tatizo kubwa kwani baada ya kutua, ilikaa muda mfupi na kuondoka tena”, amesema Madale.