Hassan Idd Kimanta aliyekuwa mlinzi binafsi wa Rais Mstaafu, Benjamin William Mkapa ambaye sasa ni Mkuu wa Mkoa wa Arusha, amesema kuwa kiongozi huyo alikuwa kama baba kwake kwa kipindi cha miaka 17.
Ameeleza kuwa aliteuliwa kuwa mlinzi wa Rais, siku moja tu baada ya Mzee Mkapa kuapishwa kuwa Rais wa Serikali ya Awamu ya Tatu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Oktoba, 1995.
“Maneno yahawezi kueleza maumivu niliyonayo sasa hivi kwa jinsi nilivyoyakosa malezi ya Mzee Mkapa. Bado namtambua kama baba hata kama amefariki dunia,” Kimanta ameiambia Daily News.
“Sitasahau pia, ulikuwa uzoefu wa aina yake kuingia Ikulu kwa mara ya kwanza, na hayo ndiyo yakawa maisha yangu kwa kipindi cha miaka 10, nikiwa na uhuru wa kuzungumza na familia ya Rais na walinichukulia kama sehemu ya familia,” aliongeza.
Mkuu huyo wa Mkoa alisema kuwa wakati wote, Mzee Mkapa alikuwa anawajali sana walinzi wake kama anavyoijali familia yake.
Ameeeleza kuwa alikuwa anaambatana na Mzee Mkapa kwa safari za ndani na safari za kidiplomasia nje ya nchi, na aliona jinsi alivyokuwa anajali hali ya utulivu wa ndani na nje ya nchi.
Moja kati ya safari alizozikumbuka sana akiwa na Mzee Mkapa, ni mkutano ambao Juba ilijitenga na Khartoum ikiwa ni matokeo ya makubaliano ya mwaka 2005 yaliyomaliza vita ya muda mrefu ya wenyewe kwa wenyewe, na jinsi alivyoshiriki katika kufanikisha makubaliano ya kugawana madaraka nchini Kenya kati ya Rais Mwai Kibaki na kiongozi wa kipindi hicho wa ODM, Raila Odinga, Februari 2008.
Katika hatua nyingine, alimkumbuka Mkapa jinsi alivyokuwa anajali uhuru wa kuabudu na kumcha Mwenyezi Mungu.
Anakumbuka jinsi ambavyo alimpa fedha kiasi cha $5,000 kujenga msikiti, baada ya kubaini kuwa mlinzi wake huyo anasali katika jengo ambalo halijakamilika.
Hata baada ya Rais Mkapa kumaliza muda wake wa kuwa Rais, Kimanta aliendelea kumhudumia kama msaidizi wake hadi alipoteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Monduli mwaka 2016.
Mzee Mkapa alifariki dunia, Julai 24, 2020 katika hospitali ya jijini Dar es Salaam alipokuwa amelazwa. Tanzania na mataifa mengine yanaendelea kuomboleza na kumkumbuka.
Mazishi yatafanyika Julai 29, 2020, Masasi, Mtwara.