Karibu watu ishirini na sita wameuwawa baada ya mlipuko katika uwanja wa ndege wa Aden huko Yemen muda mchache baada ya maafisa wa serikali mpya ya Yemen kuwasili nchini humo.
Duru za serikali na kimatibabu zimeliambia shirika la habari la Ufaransa AFP kuwa ingawa hakuna afisa yoyote wa serikali aliyeathirika zaidi ya watu hamsini ambao wamejeruhiwa.
Kipindi moshi ulipokuwa unafuka kutoka uwanja huo wa ndege huku watu wakikimbia kuwanusuru waliojeruhiwa, kulisikika mlipuko wa pili.
Mkanda wa video wa shirika la habari la AFP umeonyesha kile kilichoonekana kuwa kombora lililoulenga uwanja huo wa ndege.
Ingawa bado hakuna taarifa rasmi iliyotolewa juu ya chanzo cha mlipuko huo, baadhi ya maafisa wamewalaumu waasi wa Kihouthi wanaoungwa mkono na Iran kwa shambulizi hilo .