Kamanda wa kikosi cha usalama Barabarani nchini, Wilbrod Mutafungwa amemtaka mmiliki wa gari iliyosabababisha vifo vya watu tisa katika eneo la nanenane Manispaa ya Morogoro kujisalimisha kituo cha polisi kabla ya kesho Alhamisi, Juni 24, 2021 Saa 4 Asubuhi.
Kamanda Mutafungwa ametoa agizo hilo mara baada ya kufika katika eneo hilo ilikotokea ajali ambapo amemtaka mmiliki wa gari hilo aina ya Toyota Coaster kujisalimisha ili kutoa maelezo kwanini asichukuliwe hatua za kisheria kwa kuruhusu gari kusafiri bila kibali.
Hata hivyo, katika ajali hiyo dereva aliyesababisha ajali ni miongoni mwa watu tisa waliofariki.
Aidha Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Fortunatus Musilimu amebainisha kuwa jeshi hilo limefanya operesheni maalum na kukamata magari sita ambayo yalikuwa yakisafiri kutoka Mikoa ya Dar es Salaam na Kahama bila ya kuwa na vibali kutoka kwa mamlaka ya usafiri wa Ardhini, LATRA.