Muasisi na mmiliki wa Facebook, Mark Zuckerberg amejibu tuhuma za Rais wa Marekani, Donald Trump dhidi ya mtandao huo kuwa umekuwa na upendeleo kwa kuendesha kampeni za kumpinga siku zote.
Rais Trump ameutuhumu mtandao huo kupitia Twitter akieleza kuwa waliendesha kampeni za kumpinga kabla na baada ya uchaguzi hivyo akaubatiza jina la ‘wapinga Trump’.
Mmiliki wa Facebook amewahi kueleza wazi kuwa hampendi Trump pamoja na sera zake.
Kufuatia tuhuma hizo, Zuckerberg ameeleza kuwa anafanya jitihada zote kuhakikisha Facebook inatoa fursa kwa watu wote kuweka mawazo yao bila ubaguzi na kuwapa nguvu ya kuwasiliana moja kwa moja na wagombea.
“Facebook inawapa sauti watu wote, kuwezesha wagombea kuwasiliana moja kwa moja na wapiga kura hivyo kusaidia mamilioni ya watu kupiga kura,” BBC inamkariri Zuckerberg.
Mvutano huo umekuja wakati ambapo Facebook na Google wanatakiwa kuwasilisha ushahidi wao kwenye timu maalum ya uchunguzi kuhusu tuhuma za Urusi kuingilia uchaguzi wa urais wa Marekani mwaka 2016 uliompa ushindi Trump dhidi ya Clinton.
Facebook, Twitter na Google wote wamethibitisha kupokea mualiko wa kutakiwa kufika katika kikao cha Seneti cha Kamati ya Intelijensia kitakachofanyika Novemba Mosi mwaka huu.
Hata hivyo, hakuna aliyethibitisha kuwa atahudhuria katika kikao hicho.