Mbunge wa Kibamba (Chadema), John Mnyika, ameiomba serikali kuhakikisha inawalipa fidia wakazi wa Mloganzila ambao waliacha maeneo yao na kupisha ujenzi wa Chuo Kikuu cha Tiba na Afya Muhimbili (Muhas).
Akiuliza swali kwa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mnyika amesema baadhi ya wakazi wa eneo hilo walilipwa lakini miongoni mwao walipata kiasi ambacho hakilingani na maeneo yao, hivyo kuonekana kupunjwa.
Aidha, Mnyika ametaka kufahamu kwa jinsi gani serikali inashughulikia madai ya mapunjo ya fidia ya maendeleo kwa wakazi hao waliotakiwa kuondoka kwa ajili ya kupisha ujenzi wa Muhas.
Hata hivyo, Naibu Waziri wa wizara hiyo, Angelina Mabula, amesema ahadi ya kuwalipa fidia ya kihisani yaani mkono wa heri iliyotolewa na serikali Mei 20, mwaka juzi, itafanyika baada ya kupatikana fedha.
Mabula amesema malipo hayo hayajafanyika kwa muda kutokana na ukosefu wa fedha kwenye bajeti, lakini pale zitakapopatikana hakuna atakayeshindwa kulipwa.
Amesema tayari Serikali ilishalipa Sh. 8,067,904,700 kwa ajili ya fidia ya maendelezo ya ardhi kwa wananchi 1,919 katika kipindi cha 2008 mpaka 2010.
Aidha, amesema mwaka 2011 Serikali ilitenga Sh. 1,610,374,700 kwa ajili ya fidia ya wananchi 619 waliosalia katika malipo hayo ya fidia, wakiwa wamewekeza ndani ya shamba mali ya serikali.
Hata hivyo, Mabula ameongeza kuwa mpaka sasa Serikali haidaiwi mapunjo ya fidia kwa kuwa fidia ilikwishalipwa kwa mujibu wa sheria.